SHARE

NA WINFRIDA MTOI

MABINGWA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, wameaga rasmi jijini Dar es Salaam baada ya kumaliza mechi zake za nyumbani msimu huu na kuelekea mikoa ya Tanga na Kilimanjaro kumalizia mechi mbili zilizobaki.

Wekundu wa Msimbazi hao, wameondoka jana mchana na kikosi cha wachezaji 22, wakianzia jijini Tanga watakapocheza na Coastal Union kesho kwenye Uwanja wa Mkwakwani.

Baada ya hapo, mabingwa hao watasafiri kwenda mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu Bara msimu huu dhidi ya Polisi Tanzania Jumapili hii kwenye Uwanja wa Ushirika Moshi.

Wanamsimbazi hao wakimaliza kibarua cha Ligi Kuu Bara, wanakabiliwa na mchezo wa fainali Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), huku wakiahidi kuchukua taji hilo ili kukamilisha ndoto zao za mataji matatu kwa msimu.

Taji la kwanza la msimu huu kwa Simba ilikuwa la Ngao ya Jamii walipokutana na Azam FC, likaja la Ligi Kuu Bara, hivyo wanapigania kutwaa Kombe la Shirikisho.

Katika kuhamasisha ushindi katika michezo yao yote iliyobaki, Wekundu wa Msimbazi hao wameondoka na kombe lao la ubingwa na kuahidi watarejea Dar es Salaam wakiwa wameyashikilia mawili na lile la shirikisho.

Meneja wa timu hiyo, Patrick Rweyemanu, akielezea safari yao, alisema baada ya mechi na Coastal Union, wataelekea Kilimanjaro kucheza na Polisi Tanzania.

Alisema baada ya mechi na Polisi Tanzania ambayo itakuwa ya mwisho kwa Ligi Kuu Tanzania Bara, msimu huu, watapanda ndege kutoka Kilimanjaro hadi Mbeya ambako watapanda basi kuelekea Sumbawanga.

“Tuna safari ndefu kidogo tunapoanza kutoka hapa Dar es Salaam, itahusisha basi na ndege, ina maana Tanga na Moshi, tutatumia basi tukiwa tunaelekea Sumbawanga tutapanda ndege hadi Mbeya, kisha basi,” alisema Rweyemamu.

Alieleza kuwa maandalizi ya mchezo wao na Namungo FC wa Kombe la Shirikisho yanafanyika katika mechi mbili; dhidi ya Coastal Union na Polisi Tanzania.

“Tuko kamili, malengo yetu ni yale yale hayajabadilika, nia yetu tunataka kuchukua Kombe la Shirikisho baada ya kufanikiwa katika ligi, tunawaomba mashabiki na wapenzi, waendelee kuwa karibu na timu yao kuhakikisha wanarejea na kombe hilo,” alisema Rweyemamu.

Alifafanua kuwa wameondoka na wachezaji 22, lakini wakimaliza mechi na Polisi Tanzania, wale waliobaki Dar es Salaam watakwenda kukutana nao Mbeya na kuunganisha safari ya Sumbawanga.

Simba imefanikiwa kutwaa ubingwa kwa mara ya tatu mfululizo na sasa inajipanga kutwaa Kombe la Shirikisho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here