SHARE

NA EZEKIEL TENDWA,

SIMBA waliuanza mzunguko wa kwanza msimu huu kwa kishindo, wakiwafunga Ndanda FC mabao 3-1, lakini wakajikuta wakilazimishwa suluhu ya 0-0 na JKT Ruvu na sasa wameamua kuwaingilia na gia nyingine maafande hao mchezo wao wa mwishoni mwa wiki hii.

Wekundu hao wa Msimbazi watakuwa Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki hii kuwakabili maafande hao, huku shauku yao kubwa ni kutaka kuibuka na ushindi ili kuzidi kujikita kileleni.

Simba, ambao ni vinara wa Ligi Kuu, wanatumia zaidi mfumo wa 4-4-2, ambao ndio kocha wao Mkuu, Joseph Omog anauhusudu, lakini wanaweza wakabadilika dhidi ya JKT Ruvu na kutumia ule wa 4-2-3-1, lengo likiwa kuwamaliza wapinzani wao hao.

Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja, ameliambia DIMBA Jumatano kuwa, wanayo mifumo mingi na kama wataona inafaa wanaweza kutumia ule wa 4-2-3-1 katika mchezo wao dhidi ya JKT Ruvu, huku pia akiwatoa wasiwasi mashabiki akiwaambia kikosi kipo imara.

Kwa upande wake, Kocha Mkuu Omog alisema anachokiangalia ni pointi zote tatu na baada ya kufanya maangamizi dhidi ya Ndanda FC walipowafunga mabao 2-0, sasa ni zamu ya JKT Ruvu.

“Tumeshamaliza mchezo wetu dhidi ya Ndanda FC na jambo la kushukuru ni kwamba, tumeondoka na pointi zote tatu na sasa akili zetu tunazielekeza kwa JKT Ruvu, sisi tunacholenga ni pointi tatu, hivyo tutafanya kila linalowezekana kushinda,” alisema.

Kikosi hicho cha Simba kilitua jijini Dar es Salaam juzi kikitokea Mtwara kumenyana na Ndanda FC na jana walitarajiwa kufanya mazoezi yao Uwanja wa Polisi Kurasini, kwa ajili ya maandalizi na mchezo wao dhidi ya JKT Ruvu.

Simba wapo kileleni mwa msimamo wakiwa na pointi 38, wakifuatiwa kwa karibu na wapinzani wao wa jadi, Yanga, waliopo nafasi ya pili na pointi zao 36, ambapo Wekundu hao wa Msimbazi hawataki kupoteza mchezo wowote.

Lengo kubwa la Simba ni kuhakikisha wanatwaa ubingwa msimu huu, baada ya kushindwa kufanya hivyo kwa misimu minne mfululizo, wakiwaachia Yanga na Azam FC kubadilishana nafasi hizo za juu na kushiriki michuano ya kimataifa.

Mashabiki wa kikosi hicho wana imani kubwa kwamba timu yao msimu huu itatwaa ubingwa na kufuta machozi ya muda mrefu, hasa wakitaniwa na wenzao Yanga wakiitwa ‘Wamchangani’ na wana-Jangwani hao wakijiita ‘Wakimataifa.’

Shabiki mkubwa wa wekundu hao wa Msimbazi, Baraka Kimambo, alisema: “Hii kasi tuliyonayo kwa sasa hakuna anayeweza kutuzuia, walisema tukienda mikoani tutafungwa, lakini wenyewe wameona tulichowafanya Ndanda FC, tuna imani kubwa na kikosi chetu”.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here