SHARE

NA EZEKIEL TENDWA

HUENDA kauli hii ikawafurahisha sana mashabiki wa Simba baada ya benchi lao la ufundi chini ya kocha wao, Sven Vandenbroeck, kutamka kwamba watashusha silaha zao zote katika mchezo wa fainali, Kombe la Mapinduzi, utakaochezwa kesho Uwanja wa Amaan Zanzibar.

Mbali na kushusha silaha hizo za maangamizi, pia benchi hilo la ufundi limewaambia wachezaji wake hao kwamba lazima wamalize mchezo huo ndani ya dakika 90, tena kwa ushindi wa mabao mengi.

Kocha huyo akasisitiza kwamba, furaha yake ni kuona anashinda Kombe la Mapinduzi ili liwe taji lake la kwanza tangu alipopewa ulaji wa kuwanoa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara.

Simba wametinga hatua ya fainali baada ya kupata ushindi wa mbinde wa mabao 3-2 kwa changamoto ya mikwaju ya penalti dhidi ya Azam FC, mchezo wa nusu fainali na sasa Sven hataki tena wafike huko.

Licha ya kwamba katika mchezo huo wa nusu fainali dhidi ya Azam FC, Simba walitandaza kabumbu safu la pasi fupifupi na za uhakika, walishindwa kufunga mabao ndani ya dakika 90 kitu ambacho Sven hataki kukiona katika mchezo wa kesho.

Sven amesema wao wanataka kuchukua vikombe vyote vilivyopo mbele yao, ndiyo maana hawataki kuidharau Mtibwa Sugar na badala yake watawapangia kikosi kazi, huku akiwaambia mashabiki wakae mkao wa kula.

“Najua ni mchezo mgumu sana kama ilivyo michezo mingine lakini kutokana na upana wa kikosi changu naamini tutapata matokeo mazuri ndani ya dakika 90 tofauti na mchezo uliopita wa nusu fainali.

“Wachezaji wangu wanajua umuhimu wa kushinda mchezo huo wa fainali kwani malengo yetu ni kutwaa vikombe vingi kadri tutakavyoweza na tunataka mwaka huu tuanze na hiki cha Mapinduzi,” alisema kocha huyo raia wa Ubelgiji.

Kwa upande wake, kocha msaidizi wa Simba, Selemani Matola, akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo wao wa nusu fainali dhidi ya Azam FC, alisema wanafahamu Mtibwa Sugar ni timu nzuri na yenye nia ya kutwaa ubingwa huo, lakini hao hawatawapa nafasi.

“Mtibwa Sugar ni moja ya timu ngumu sana kutokana na kucheza kandanda la kuvutia lakini ninaamini sisi tupo vizuri zaidi yao na bila shaka tutapata ushindi na kutwaa ubingwa wa michuano hii ya Mapinduzi,” alisema.

Mashabiki wa Simba nao hawakuwa nyuma katika kuizungumzia timu yao ambapo Eli Kikwesha au Mzee Vuvuzela, alisema kikosi kilichopo Zanzibar ni cha mauaji na anaamini watapata ushindi mnono dhidi ya Wakata Miwa hao kutoka Turiani, Morogoro.

“Awali walivyowaacha kina Kagere (Meddie) na Chama (Clatous) Dar es Salaam, nilipatwa na wasiwasi lakini walivyokwenda roho yangu ilitulia, naamini Mtibwa Sugar tutawafunga mabao mengi sana,” alisema.

Wakati Simba wakijigamba kutwaa ubingwa huo, msemaji wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru, ameibuka na kudai kuwa wao Zanzibar ni kama wenyeji hivyo lazima wawaadabishe Wekundu hao wa Msimbazi.

Simba wametinga hatua hiyo baada ya kuwafunga Zimamoto mabao 3-1 na baadaye kuwafunga Azam FC mabao 3-2 kwa mikwaju ya penati huku Mtibwa Sugar wao wakitinga hatua hiyo wakiwafunga Chipukizi mabao 4-2 kwa mikwaju ya penati baada ya dakika 90 kumalizika sare ya bao 1-1 kabla ya kupata tena matokeo kama hayo dhidi ya Yanga mchezo wa nusu fainali.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here