SHARE

NA MWANDISHI WETU

JEURI ya fedha haijawahi kumuacha mtu salama. Hii ni baada ya Simba kutaka kuwakomba mastraika wote walioongoza kwenye mbio za ufungaji msimu huu uliomalizika.

Katika orodha hiyo ya wafungaji, straika Mganda, Emmanuel Okwi, ndiye anayeongoza, akiwa na mabao 20, akifuatiwa na mwenzake, John Bocco, mwenye mabao 14, wote hao wakiwa ni wachezaji wa Simba.

Sasa unaambiwa wale wote wanaowafuatia kwa karibu baadhi yao tayari wameshamwaga saini katika Klabu hiyo, huku viongozi wakiendelea na mazungumzo na wengine.

Tayari Marcel Kaheza wa Majimaji, ambaye ana mabao 14 sawa na Bocco, ameshasaini Simba, huku Obrey Chirwa wa Yanga ambaye anafuatia akiwa na mabao 12, naye akiwa anawindwa kwa muda mrefu na haitashangaza akisaini.

Kama ulidhani wameishia hapo, utakuwa hujui kinachoendelea, kwani taarifa zaidi zinadai kuwa, hata yule mkali wa mabao wa Tanzania Prisons, Mohamed Rashid, anayeshika nafasi ya tano, ameshawekwa kwenye rada muda mrefu.

Straika huyo wa maafande hao wa jijini Mbeya, yupo nyuma ya Chirwa, akiwa amefunga mabao tisa na huenda Simba wakafanya kweli kama walivyomsainisha kiaina Adam Salamba na kuwazidi kete Yanga na Azam, waliokuwa wakimuwinda straika huyo kutoka Lipuli FC.

Simba wamepania kufanya usajili wa nguvu wakijua kuwa, wanakabiliwa na michuano migumu ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku wakijua kuwa wamepewa mtihani mkubwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, aliyewaambia wahakikishe wanalileta kombe hilo hapa nchini.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here