SHARE

MANCHESTER, England

OLE Gunnar Solskjaer ameshindwa kumnyamazia kimya Robin van Persie baada ya straika huyo wa zamani wa Man Utd kumponda kocha huyo kwa kitendo chake cha kutabasamu kufuatia kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Arsenal.

Van Persie alimtupia lawama Solskjaer kwa aina ya soka analofundisha, lakini pia ‘alimpa’ ushauri kocha huyo kuonyesha sura ya hasira baada ya matokeo mabovu hasa yale ya juzi dhidi ya Arsenal.

Mara baada ya kumalizika kwa mechi hiyo, Solskjaer alionekana kuwa na tabasamu pana usoni wakati akifanyiwa mahojiano kitu ambacho hakikumfurahisha Van Persie ambaye alialikwa kuwa mchambuzi katika kituo cha runinga cha BT Sport.

“Solskjaer anaonekana kuwa mtu mzuri sana, lakini ningependa awe anaonyesha hali fulani ya mtu asiyetaka kushindwa, aonyeshe hasira…Nikimtazama sasa namuona anatabasamu baada ya mechi, huu si wakati muafaka wa kutabasamu,” alisema Van Persie.

Hata hivyo, Solskjaer aligeuka mbogo juu ya kauli hiyo ya RVP na kusisitiza kuwa hatabadilisha aina ya soka analofundisha Old Trafford.

“Simjui Robin na Robin hanijui mimi,” alisema Solskjaer.

“Kiujumla hana haki ya kulaumu aina ya ufundishaji wangu na sitabadilika. Nafahamu kuwa aliirithi jezi yangu namba 20, lakini hawezi kuvuka zaidi ya hapo,” alisikika akisema Solskjaer huku akiondoka kwenye mkutano na waandishi wa habari.

Wakati huo huo, Januari ya mwaka 2020 ndio hiyo imeanza kurindima na ni kipindi cha usajili, lakini Man United tayari imemkosa mmoja wa wachezaji ambao inawahitaji ambaye ni Erling Braut Haaland.

Straika huyo kinda raia wa Norway ametua Dortmund akitokea RB Salzburg na imebainika kuwa Man Utd ilitaka kumchinjia baharini wakala wake, Mino Raiola, mpango ambao ulishindikana.

Haaland alikuwa ni mchezaji wa kwanza aliyetakiwa United, lakini klabu hiyo iliamua kujitoa baada ya kushindwana na Raiola ambaye anasifika kwa kujichotea fedha nono katika dili za usajili. 

Kwa mujibu wa mtandao wa Daily Mail, Man Utd ilitaka kufanya biasharana baba wa mshambuliaji huyo, kiungo wa zamani wa Leeds Utd, Alf Inge Haaland ambaye naye ni wakala wake. 

Hata hivyo, jaribio hilo la United liligonga mwamba na Haaland ameishia kusaini Dortmund kwa dau la uhamisho la pauni milioni 18.

Pia, Dortmund imekubali kuwapa Raiola na baba wa Haaland mgawo wa fedha pindi straika huyo atakapouzwa ikiwa na maana kwamba wakala ndiye mwenye nguvu katika dili za usajili zitakazomhusisha Haaland kitu ambacho Man Utd haikuwa tayari kukubaliana nacho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here