SHARE

LONDON, England

MARA baada ya kushuhudia mchezo mkali wa nusu fainali ya kwanza ya Kombe la FA iliyochezwa usiku wa kuamkia leo kati ya Arsenal na Manchester City ndani ya Uwanja wa Wembley.

Basi, muendelezo wa mechi ya pili ya nusu fainali utafanyika leo ndani ya uwanja huo mkubwa nchini England, kwa kuzikaribisha klabu za Manchester United na Chelsea.

Timu hizo zimepishana pointi moja tu katika msimamo wa Ligi Kuu England na wanaenda kukutana wakitoka kushinda michezo yao kwenye ligi.

Huu utakuwa mchezo wa nne kwa vigogo hao wa soka England kucheza msimu huu. Mechi tatu za awali zilizopita, Manchester United walikuwa wababe wa Chelsea.

Mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu msimu huu, vijana wa Ole Gunnar Solskjaer waliisambaratisha Chelsea kwa mabao 4-0, kisha kuwaondoa katika Kombe la Ligi kwa mabao 2-1, kabla ya kushinda mabao 2-0 kwenye mechi ya pili ya Ligi Kuu.

Kocha wa Manchester United, Solskjaer amesema kikosi chake kipo tayari kucheza dhidi ya wapinzani wao, ingawa, wamepata muda mdogo wa kupumzika.

“Kila mmoja anajua umuhimu wa mchezo huo wa FA, hauwezi kuwa rahisi kwa timu zote mbili, Chelsea ni timu nzuri, wamekuwa bora tangu ligi iliporejea.

“Tupo tayari, wachezaji wapo vizuri na wanatamani kucheza tena, tutapumzika kwa saa 48 kabla ya kuingia uwanjani tena, hatuwezi kuwa na kisingizio.

“Njaa ya mafanikio ni kitu kikubwa kwa wachezaji wetu, kila mmoja anayepata nafasi anataka kuonyesha kuwa ni mtu sahihi wa kuendelea kuwepo Manchester United.

“Hii ni timu inayopigania vikombe, bila kujali ukubwa au udogo wake, FA ni taji lenye historia kubwa hapa England, tunahitaji kuwa sehemu ya historia kwa kushinda msimu huu,” alisema.

Naye, Lampard anaamini huu ni wakati sahihi wa timu yake kulipa kisasi kwa Manchester United ambayo imewanyanyasa katika mechi tatu zilizopita.

“Tunajua ni timu iliyokusanya wachezaji wenye uwezo mkubwa, tutapambana kutinga fainali sababu mchezo hautokuwa rahisi,” alisema.

Kwa pamoja, Man United na Chelsea zimekusanya mataji 20 ya Kombe la FA. Yaani United wanayo 13 na Blues wameweka saba kwenye kabati lao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here