SHARE

NEW YORK, MAREKANI

UKIYATAJA majina matano ya mastaa wa kikapu ambao wanacheza Ligi ya NBA, hauwezi kuliacha jina la Stephen Curry ambaye anakipiga katika timu ya Golden State Warriors, aliyezaliwa Machi 14, 1988, Akron, Ohio huko nchini Marekani.

Majina makubwa mengine kwenye mchezo huo ni pamoja na Michael Jordan, Shaquille OíNeal, LeBron James, marehemu Kobe Bryant, Kevin Durant na wengine wengi, lakini kwa sasa Curry anatajwa kuwa mmoja kati ya mastaa ambao wanapendwa sana na idadi kubwa ya mashabiki.

Staa huyo mwenye miaka 32, hadi sasa ana jezi moja tu ya timu ya Golden State Warriors ambayo alianza kuitumikia tangu mwaka 2009, hiyo ni klabu yake ya kwanza na hajawahi kuitumikia timu nyingine.

Anatajwa kuwa mchezaji ambaye hana mambo mengine mengi ya kumfanya awe na jina kubwa ndani ya uwanja, ila ni kiwango chake tu kutokana na mazoezi ya kila siku na kuujua mchezo huo tangu akiwa na umri mdogo.

Yafuatayo ni mambo matano ambayo hauyajui kuhusu Stephen Curry ambaye amekuwa na mchango mkubwa wa mafanikio ya timu hiyo kwa kipindi cha miaka kadhaa.

Alianza kikapu akiwa na miaka mitano

Hii inaonesha ndio sababu kubwa ya kuwa staa kwa sasa kwenye mchezo huo katika Ligi ya NBA nchini Marekani. Aliacha kucheza akiwa na miaka mitano kwa kuwa baba yake Dell alikuwa mchezaji wa timu ya Charlotte Hornets, hivyo muda mwingi alikuwa anamchukua Curry pamoja na mdogo wake Seth kwenye michezo yao.

Curry alianza kuupenda mchezo huo mbali na kushuhudia michezo mbalimbali lakini alikuwa anamuona baba yake akifanya mazoezi nyumbani.

Kwenye gofu pia yupo

Mbali na kuwa bora kwenye mchezo wa kikapu, lakini anatajwa kuwa bora kwenye mchezo wa gofu. Kipindi ambacho NBA ipo kwenye mapumziko nyota huyo anatumia muda huo kushiriki michuano mbalimbali ya mchezo wa gofu.

Mchezo huo alikuwa anacheza sana wakati yupo shule. Katika mashindano ya gofu kwa mastaa mchezaji huyo amekuwa akiwakimbiza wanzeka.

Aliyewahi kuwa rais wa Marekani, Barack Obama, amekuwa akimwalika mchezaji huyo nyumbani kwake kwa ajili ya kushindani mchezo huo.
Hii ndio sababu ya kuvaa namba 30

Baba wa mchezaji huyo Dell alikuwa nyota wa kikapu miaka ya nyuma japo hakuwa kwenye kiwango kikubwa kama ilivyo kwa Curry, lakini Dell alikuwa anavaa jezi namba 30.

Kutokana na hali hiyo hata Curry alikuwa anavalishwa jezi namba 30 kila wakati anapokwenda kuangalia michezo mbalimbali, hivyo ikamfanya mchezaji huyo kuamua kuchukua namba hiyo moja kwa moja kwa ajili ya kumuenzi baba yake.

Anapenda kusaidia jamii

Curry amekuwa akipambana kuhakikisha kile anachokipata katika mafanikio yake kiasi fulani kitumike kwa jamii, hivyo ni mmoja kati ya mabalozi wa kupambana na Maralia duniani.

Mwaka 2013, mchezaji huyo alikuja nchini Tanzania akiwa na kampeni yake ya kupambana na Malaria ambayo ilikuwa inajulikana kwa jina la Nothing But Nets

Mama anachangia kiwango cha Curry

Ni wazi kwamba mama wa staa huyo ambaye anajulikana kwa jina la Sonya, anahusika kuchangia kiwango cha staa huyo kuwa juu kwa kuwa wamekubaliana kuwa, endapo Curry kwenye mchezo wake atasababisha timu yake kufungwa pointi moja basi atatakiwa kulipa faini ya dola 100, ambazo ni sawa na 230,678 za Kitanzania. Curry anapambana kuhakikisha asifanye makosa na kulipa faini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here