SHARE

NA MAREGES NYAMAKA,

VUTA nikuvute kati ya miamba miwili ya soka nchini, Simba na Yanga, kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara iliendelea mwishoni mwa wiki hii, huku vigogo hivyo vyote vikiibuka na ushindi katika mechi zao za mwishoni mwa wiki.

Yanga ilifanikiwa kuichakaza Tanzania Prisons kwa mabao 2-0 yaliyowekwa kimiani na Amis Tambwe pamoja na Obrey Chirwa, ambao wamefunga katika michezo miwili mfululizo ya ligi hiyo, huku mahasimu wao Simba wakifanikiwa kulipa kisasi dhidi ya African Lyon kwa kuwapa kichapo cha mabao 2-1 na kurejea tena kileleni kufuatia kufikisha pointi 62, baada ya kucheza mechi 28 wakiwarudisha nafasi ya pili mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 59 za mechi 26, kabla ya Wanajangwani hao kucheza na Kagera Sugar jana Jumanne.

Lakini pia Azam FC waliendeleza  rekodi yao bora  katika Uwanja wake wa Azam Complex  kwa kutopoteza mchezo hata mmoja, ikiwa ni baada kuibuka kidedea kwa ushindi wa mabao 3-1 mbele ya wabishi Mbao FC.

Ukiweka pembeni  timu hizi kubwa zilizopata matokeo bora katika michezo hii ya lala salama, lakini pia kuna wanandinga ambao wamefanya vizuri sana msimu huu katika vikosi mbalimbali  vya ligi hiyo na ambao huenda wakawashawishi Simba, Yanga na Azam kuwavuta vikosini mwao msimu ujao.

Ni jambo lililo dhahiri kwamba katika timu zote 13 kati ya 16 za Ligi Kuu Tanzania, mchezaji akifuatwa na timu hizo tatu vigogo katika kipindi kijacho cha usajili na ikitokea akazigomea timu hizi, kuna mambo mawili nyuma yake, kwamba ama  nyota huyo atakuwa anachezea timu ya Jeshi ambayo imemwajiri pande mbili, pia dau kubwa lisiloendana na uhalisia.

Kutokana na uhalisia jinsi ulivyo, nyota wafuatao huenda wakatupiwa macho zaidi na klabu hizo tatu kwa ajili ya kufanya nao mazungumzo ili wazitumikie msimu ujao kutokana na mavitu waliyoyaonyesha katika timu zao msimu huu.

Mabeki

Moja kati ya mabeki wa pembeni ambao wamefanya vizuri sana msimu huu ni Salum Kimenya anayekipiga katika klabu ya Tanzania Prisons ya Mbeya na Adam Miraji wa African Lyon, ambapo wawili hao wamekuwa na mchango mkubwa kwenye vikosi vyao hivyo.

Kimenya ambaye ameendeleza ubora wake kama ilivyokuwa msimu uliopita akiwa chini ya Salum Mayanga, aliwatoa Simba udenda ambapo Wekundu hao wa Msimbazi waligonga mwamba kwa kushindwa kuweka mezani  dau la shilingi milioni 60 alilolihitaji nyota huyo.

Hata hivyo, Simba huenda wakarejea kwa mara nyingine kumshawishi kutua Msimbazi kusaidiana na mkongwe  Janvier Besala Bukungu kwenye nafasi ya beki wa kulia, kutokana na ukweli kwamba beki mwingine aliyeko kwenye kikosi hicho, Hamad Juma, ameshindwa kung’ara na hivyo kujikuta akikosa namba.

Nyota mwingine ambaye ‘zali’ huenda likamwangukia kama ikishindikana kwa Kimenya ni Miraji Adam, kinda wao wa zamani anayeendelea kufanya mambo makubwa kwenye kikosi cha African Lyon waliomsajili kutoka katika kikosi cha Coast Union ya mkoani Tanga.

Viungo

Ukiondoa viungo wazawa wenye uwezo mkubwa kama kina Juma Said Makapu (Yanga), Jonas Mkude, Mzamirru Yassin na Said Ndemla (Simba) pamoja na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Hidmid Mao wa Azam, ambao wana uhakika wa namba kwenye vikosi vyao, pia msimu ujao wanaweza kuungana na kina Rafael Daud na Kenny Ally; wote wa Mbeya City.

Wawili hao ni miongoni mwa wazawa wanaocheza nafasi ya kiungo ambapo wamekuwa gumzo kutokana na umahiri wao uwanjani, ikiwamo kuonyeshana umwamba mbele ya  wazawa hao wenzao wa timu kubwa.

Rafael Daud aliyewahi kufukuziwa na Yanga msimu uliopita, uimara wake umeongezeka mara dufu ikiwamo kuingia wavuni mara tisa, chachu inayompa thamani zaidi sokoni huku mwenyewe akiwa tayari kukipiga hapo kwa Wanajangwani akichagizwa na kuwa kama mchezaji huru.

Kwa upande wa Keny Ally mwenye mkataba wa mwaka mmoja na Mbeya City, tayari tetesi za usajili zinamhusisha kujiunga na Yanga msimu ujao, baada ya Wanajangwani hao kuridhishwa na uwezo wake mkubwa wa kumiliki mpira, huku pia akionyesha nidhamu ya hali ya juu uwanjani katika suala zima la kukaba na kupokonya mipira kwa adui.

Mastraika

Ukiangalia msimamo wa wachana wavu kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, utabaini kuna  mastraika wawili nje ya Simba, Yanga na Azam, ambao ni Abdurahman Mussa wa Ruvu Shooting na Mbaraka Yusuph wa Kagera Sugar walioingia wavuni mara 12 kila mmoja.

Kutimiza kwao jukumu lao hilo mama kunawafanya kuwa na wastani mzuri wa kufunga kama ilivyo kwa mastraika wengine ulimwenguni kote na kuwafanya wawe ‘dili’ katika kipindi cha uhamisho, ambapo huenda wakatakiwa na timu kubwa.

Hatua hiyo inawafanya kuwa na nafasi nzuri ya kuwindwa na timu hizo tatu vigogo, Mbaraka akianza kuhusishwa na klabu yake ya zamani Simba, inayomuwinda ili imrejeshe kwenye himaya yao.

Hata hivyo, kwa upande wa Abdurahman Mussa, inavyoonekana ni kwamba timu sahihi ambayo anaweza kuichezea kutokana na aina yake ya uchezaji ni Azam FC, kwani hakuna presha kubwa  ya mashabiki kama zilivyo Simba na Yanga.

Lakini pia kama walivyodhamiria Azam wanaweza kumchukua fasta ili kuimarisha kikosi cha kufanya usajili wa nguvu hasa safu ya ushambuliaji ilionekana butu kiasi flani msimu huu, mkombozi pekee akiwa John Bocco hadi sasa akifunga jumla ya mabao 10.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here