SHARE

NA MAREGES NYAMAKA

KATIKA soka, timu inavyokuwa na machaguo ya kwanza katika kikosi cha kwanza ambao ni wachezaji wapya, lazima neno ‘subira’ liwepo kwa ajili ya kuwapa muda wachezaji, ili kuendana na falsafa ya sehemu husika, ikichagizwa pia na mbinu pamoja na mifumo ya kocha.

Lakini pia kwa upande wa pili huenda kusiwepo na nafasi ya neno hilo la kumpa muda mchezaji kama wachezaji hao wataingia haraka kwenye mfumo na kuwasha moto kama walivyokuwa kwenye vikosi vyao vya awali.

Kwa miaka kadhaa sasa, suala la kubadili badili vikosi lilikuwa likiisumbua mno timu ya Simba, ambayo licha ya kuwa na machaguo mengi ya wachezaji kwa wakati mmoja, lakini benchi la ufundi la timu hiyo lilikuwa ikipata shida kujenga upya kikosi chake kila msimu kutokana na timu kubomoka.

Suala kama hili limewakuta pia watani zao wa jadi, Yanga, msimu huu, ambao kwa asilimia kubwa kikosi cha timu yake ni kama kipya, baada ya wachezaji wengi wa zamani, tena wale tegemeo, kutimka mara baada ya msimu uliopita kumalizika.

Yanga msimu huu imeonekana kuwa na machaguo mapya kwenye kikosi chao cha kwanza, tofuati kabisa na misimu kadhaa iliyopita.

Hata hivyo, licha ya kuwa walikuwa wakifanya usajili mpya karibu kila msimu, lakini wachezaji wapya waliokuwa wakisajiliwa hawakufikia viwango vya kuwachomoa kikosi cha kwanza nyota waliowakuta.

Baada ya kuondokewa na wachezaji wake tegemeo wa kikosi cha kwanza kipindi cha dirisha la usajili la msimu huu, Wanajangwani walilazimika kuingia sokoni kwa nguvu kusaka mbadala sahihi wa nafasi hizo.

WALIOONDOKA, WALIOINGIA

Nyota tegemeo waliotimka katika viunga hivyo vya Jangwani na ambao walikuwa chachu ya Yanga kutwaa taji hilo kwa mara tatu mfululizo msimu uliopita walikuwa ni kipa Deogratius Munishi ‘Dida’, beki wa kati Mtogo Vicent Bussou, kiungo fundi wa mpira Haruna Niyonzima pamoja na mfungaji bora Simon Msuva.

Ikumbukwe katika kundi la nyota hao aliyewashangaza wengi mwanzoni ni Bussou, kutokana na kusugua benchi kwa muda mrefu na kuanza kuzua mijadala, lakini ilipotokea kupewa nafasi kwenye kikosi cha kwanza aliitendea haki nafasi hiyo kuanzia hapo na hadi anatimka alikuwa akitazamwa kama lulu.

Nafasi zao kwenye kikosi cha kwanza zimechukuliwa na mlinda mlango Youthe Rostand, viungo Rafael Daud na Mcongo Pappy Kabamba Tshishimbi, pamoja na beki wa kushoto Gadiel Michael.

Wakali hawa wanne ambao wameingia kwenye kikosi cha kwanza cha kocha Mzambia, George Lwandamina, walikuwa wakitesa kwenye vikosi vyao walivyotoka.

WALIVYOFANIKIWA

Kati ya walioingia, ni Tshishimbi na Gadiel Michael ndio walioanza vema zaidi kuonyesha mwanga wa mapema kuashiria kung’ara katika mikono ya Lwandamina ndani ya falsafa za Yanga.

Na kama beki wa kushoto, Gadiel Michael ataendeleza umahiri wake katika mechi tano zijazo, ni dhahiri anaweza kabisa kumpoka namba beki aliyekuwa akicheza namba hiyo, Haji Mwinyi Mngwali, ambaye huenda akawa chaguo la pili akitokea benchi kulingana na mahitaji ya kocha.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba Gadiel anajua jinsi ya kukaba, kupanda mbele kusaidia mashambulizi na kupiga krosi sahihi zinazowafikia mastraika.

Naye kiungo Mcongoman Tshishimbi, anaonekana dhahiri kutibu donda sugu la Yanga kwenye nafasi ya kiungo mkabaji na ameimudu nafasi hiyo vizuri zaidi kuliko alivyokuwa Frank Domayo, misimu mitatu iliyopita, kwani kila mmoja ameonekana kuridhishwa na uwezo wake.

Lakini bado ni mapema mno kumpa asilimia 100, kwa kuwa anahitaji muda zaidi kuizoea ligi yenyewe, jiografia ya maeneo, hususan viwanja, hasa vya mikoani ambavyo changamoto yake inajulikana, lakini pia kuwa na muunganiko wa timu nzima kwa ujumla.

Hata hivyo, huenda akapita kwenye nyayo za akina Mbuyu Twite, Donald Ngoma na Thaban Kamusoko, waliyoizoea ligi na mazingira  kwa ujumla na kufanikiwa kuwa uti wa mgogo wa timu.

Kwa upande wake Rafael Daudi, ambaye ni mzawa na mzoefu wa ligi, ana nafasi kubwa ya kurithi mikoba ya Simon Msuva kwenye nafasi ya winga ya kulia, kama kocha ambavyo ameanza kumtumia katika mazoezi hivi karibuni kutoka kumchezesha kama nambo 10 alipocheza michezo miwili ya Simba na Lipuli.

Kujiamini kwa Daudi namna anavyokuwa na mpira mguuni, kukokota kwake na kutoa pasi kwenda kwa mlengwa, kama ataondoa presha ya mashabiki kutoka jukwaani kama ilivyowakumba wachezaji kadhaa waliyoshindwa kumudu hilo jambo, huenda akawa lulu mahali hapo.

Kwa upande wa Mcameroon, Rostand, aliyechukua mikoba ya Dida, yeye anatazamwa kama Yaw Berko mpya katika viunga hivyo, kulingana na utendaji wake wa kazi yake, akichagizwa pia na umbo lake kubwa. Hata hivyo, anaweza kutoa taswira halisi baada ya michezo mitano na kuendelea.

Mbali na akina Twite na Kamusoko, mchezaji mwingine aliyeingia katika kikosi cha Yanga na kung’ara moja kwa moja akitesa vilivyo katika kikosi cha kwanza ni Deus Kaseke, aliyetokea Mbeya City, chini ya Hans Van Pluijm, kabla ya ujio wa kocha wa sasa, Lwandamina.

WALIOFELI

Ukimuacha Justin Zulu, aliyesajiliwa na Lwandamina na kushindwa kung’ara kwa kiasi kikubwa katika kikosi hicho na hivyo kujikuta akitupiwa virago, lakini pia kuna kundi la wachezaji wengine huko nyuma walioonyesha cheche katika ligi na ndani ya timu za awali na kuwavutia Yanga, lakini walipotua Jangwani maji ‘yakazidi unga’, nikimaanisha kushindwa kuonyesha uwezo.

Said Bahanuzi, aliyeanza kwa kishindo michuano ya Kombe la Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame na kufanikiwa kutwaa kiatu cha dhahabu siku chache baada ya kumwaga wino kuitumikia Yanga, lakini baada ya ligi kuanza mambo yakaenda kombo na msimu uliofuata akapewa mkono wa kwaheri.

Wengine walioshindwa kung’ara katika vikosi tofauti tofauti vya Wanajangwani ni Hussein Javu, Rashid Gumbo, Danny Mrwanda, Shaaban Kondo, Hamis Thabiti na mchezaji msomi zaidi, Reliants Lusajo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here