SHARE

LIGI Kuu Tanzania Bara inatarajia kuanza Jumamosi ijayo kwenye viwanja mbalimbali Tanzania Bara. Ligi ya msimu huu imekuja ikiwa na timu moja ngeni kwenye ligi hiyo ambayo ni Njombe Mji.

Pia zipo timu nyingine mbili zilizopanda daraja kutoka la kwanza hadi Ligi Kuu ambazo ni Lipuli ya Iringa, Singida United ambazo miaka iliyopita zilishawahi kushiriki ligi hii.

Jambo kubwa ambalo ninaliona kwa wakati huu hasa kwa utawala mpya wa soka chini ya Rais Wallace Karia, ni kuhakikisha kuwa yale mambo ambayo yamekuwa yakijitokeza na kulalamikiwa kwa miaka mingi tangu uhuru wa Tanganyika, yanafanikiwa kwa kushirikiana na waendeshaji wa ligi hiyo, Bodi ya Ligi.

Mambo yanayolalamikiwa na yanayokwamisha maendeleo ya Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo kimsingi yanajulikana ingawa si mbaya kukumbushana kwa ajili ya maslahi ya wote ili soka la Tanzania lisonge mbele.

Ratiba ya ligi hii imekuwa haitabiriki na kwa sababu leo inaweza ikawa iko hivi, lakini ndani ya muda mfupi ikapanguliwa jambo ambalo kwa sehemu kubwa limekuwa likilalamikiwa na makocha na viongozi wa timu kuwa imekuwa ni kikwazo katika kupanga taratibu na ratiba bora ya timu zao.

Inawezekana kupangua pangua huku kunatokana na michuano mbalimbali ambayo Tanzania inapaswa kushiriki, lakini ukweli uliopo ni kwamba ratiba za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na lile la Kimataifa (FIFA) zinafahamika, hivyo lazima zifuatwe na isiwe ni jambo la dharura au zimamoto.

Hii ina maana kwamba kama taraifa hizo na mipangilio mingine ikijulikana mapema, ni wazi kwamba tunaweza kuwa na ligi bora yenye ushindani kwa sababu timu zitakuwa zimejipanga vizuri zaidi na hapatakuwa na kuyumbishana kama ambavyo baadhi ya timu zimekuwa zikilalamika.

Kuwepo kwa ratiba imara ina maana kwamba kila kitu kitakwenda sawa, mshindi atapatikana katika mazingira ambayo ni ya haki kwa kila mtu lakini hata timu ikishuka daraja haitakuwa na kisingizio kuwa mazingira ya ratiba kwenye ligi hayakuwa rafiki, hilo ndilo ambalo naamini linaweza kufanyika tukatoka hapa tulipo na kwenda mbele.

Suala la nidhamu kwa timu zetu nalo limekuwa ni changamoto. Jambo hili limekuwa likiwalenga moja kwa moja wachezaji na baadhi ya viongozi na mashabiki katika timu za Ligi Kuu.

Wapo wachezaji ambao hawaamini katika kusimamia sheria na kanuni za ligi pamoja na sheria 17 zinazosimamia mchezo wa soka, ila wanataka kufanya wanayoona yanastahili jambo ambalo kimsingi linaondoa ladha na heshima ya mchezo wa soka.

Kwa mantiki hiyo, ni lazima TFF kwa kushirikiana na Bodi ya Ligi kufuata sheria na kanuni walizojiwekea sambamba na kuongeza ukali wa adhabu kwa timu zitakazoonekana kuvunja sheria au watu watakaoonekana kuwa kikwazo katika maendeleo kwenye ligi.

Japo kwa siku za karibuni hatujaona likitokea, lakini wapo waamuzi walishawahi kupigwa na wachezaji katika miaka iliyopita, lakini wengine walipigwa na mashabiki. Hili jambo halikubaliki kwa sababu linavunja haki za waamuzi lakini vile vile inawanyima haki wadau wa soka kuwepo kwenye mchezo huo ambao unaongoza kwa kupendwa duniani.

Suala la nidhamu ni muhimu kwani bila nidhamu hakuna mashindano, kwa sababu hiyo waamuzi nao wanastahili kupewa haki yao na heshima yao kutokana na kazi kubwa wanayoifanya kusimamia na kutoa haki kwa timu zinazoshindana, naamini hiyo ndiyo heshima pekee ambayo anastahili kupewa mwamuzi na si kitu kingine chochote.

Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali zinaonyesha kwamba ligi yetu pamoja na kuwa inalipa kuliko nyingine Afrika Mashariki, lakini pia kuna tatizo kubwa la rushwa.

Wapo baadhi ya wachezaji kutoka kwenye baadhi ya timu wamekuwa ni vinara wa kupanga matokeo baada ya kupewa rushwa, jambo ambalo wakati mwingine husababisha kuwepo kwa bingwa dhaifu ambaye akienda kwenye michuano ya kimataifa hafanyi vizuri kwa kuwa amepatikana kwa njia zisizofaa kulingana na sheria za soka.

Rushwa mara kadhaa imesemwa na wachezaji, makocha na wadau wengine wamekuwa wakilalamikia jambo hilo lakini halijaweza kufanyiwa kazi ipasavyo. Hivyo, TFF na Bodi ya Ligi wanaweza kujiandaa vyema na jambo hilo kwa kushirikiana na wadau wengine ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), ili kufuatilia ukweli wa mambo yanayosemwa hata kama ni porojo.

‘Saratati’ hii kwenye soka la Tanzania ikiweza kumalizwa ni wazi kuwa tutaweza kuona ushindani bora zaidi kwenye ligi yetu, ambayo utaweza kusaidia kupata bingwa wa ukweli kwenye uwezo anayeweza kushindana kimataifa bila kujua ni timu gani imetwaa ubingwa.

Waamuzi nao hawajaachwa nyuma kwa sababu ni kundi ambalo limekuwa likilalamikiwa na kwamba limechangia kuzorotesha ligi kwa kile kinachoelezwa kuwa ni uwepo kwa uchezeshaji ligi usiozingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa jambo ambalo ni baya kwa maendeleo ya soka la Tanzania.

Haya ni mambo ambayo yakimulikwa vyema na kushughulikiwa yataweza kusaidia katika maendeleo ya soka la Tanzania, kwani hayo ndiyo maeneo yanayosemwa zaidi na wadau wa soka la Tanzania.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here