SHARE

LONDON, England

KAMA ilivyo kawaida ya Premier League, Januari huwa ni wakati wa mashabiki wa soka kupata taswira ya namna msimu utakavyomalizika itakapofika mwezi Mei.

Nani atabeba taji, wangapi watamaliza ndani ya ‘Top 4’, nani atafuzu Europa na nani atashuka daraja? Haya ni baadhi ya maswali ambayo wapenzi wa EPL huanza kujiuliza wakati huu.

Chelsea wameendelea kukomaa kileleni japo walionekana kupoteza uhakika wa ubingwa baada ya kuchezea kichapo cha kushtukiza cha bao 2-0 kutoka kwa Tottenham Hotspurs.

Pia habari za Diego Costa kugomea mazoezi zinaivuruga kambi ya vijana wa Antonio Conte, kwa kuwaza namna watakavyocheza bila straika wao aliye kwenye kiwango bora msimu huu.

Lakini Chelsea walijibu maswali yote hayo baada ya kuichapa Leicester bao 3-0 bila ya Diego Costa, ushindi huu ukarudisha matumaini yao ya kubeba taji msimu huu.

Makala haya yamekuandalia uchambuzi wa timu 6 za juu zinazoonekana kugombea taji na nafasi ya kufuzu ligi ya mabingwa msimu ujao.

Chelsea – Nafasi ya 1

Kiwango chao: Wameshinda mechi 14 kati ya 15 walizocheza hivi karibuni.

Ratiba: Januari 22 – Hull (nyumbani), Januari 31 – Liverpool (ugenini), Februari 4 – Arsenal (nyumbani).

Conte alifanya kazi kubwa ya kurejesha morali kwenye kikosi chake mara baada ya kupokea kichapo cha bao 2-0 kutoka kwa Tottenham, akatulia na kujipanga upya.

Lakini kwa bahati mbaya zaidi wakati akitafakari namna ya kuunda upya makali ya kikosi chake, straika wake Diego Costa, akagoma kufanya mazoezi na timu na akakosekana kwenye safari ya mchezo wa ugenini dhidi ya Leicester, katika dimba la King Power.

Wengi wakiamini kuwa huu ungekuwa mwisho wa ngebe za Chelsea, Conte akafanya mabadiliko machache kwenye kikosi chake kwa kumwanzisha Mbrazil, Willian aliyecheza sambamba na Pedro na Eden Hazard katika safu ya ushambuliaji.

Mabadiliko hayo yakazaa matunda kwa Chelsea kuibuka na ushindi mnono wa bao 3-0 ugenini na kubeba pointi tatu muhimu zilizowaweka kwenye mazingira mazuri katika safari yao ya ubingwa msimu huu.

Lengo: Watamaliza ndani ya ‘Top 4’, wana nafasi kubwa ya kubeba taji.

Tottenham – Nafasi ya 2

Kiwango chao: Wameshinda michezo yote 6 ya hivi karibuni.

Ratiba: Januari 21 – Manchester City (ugenini), Januari 31 – Sunderland (ugenini), Februari 4 – Middlesbrough (nyumbani).

Kikosi cha Mauricio Pochettino kimeendelea kuonyesha kuwa wako ‘siriaz’ na ubingwa msimu huu baada ya kuichapa West Bromwich Albion bao 4-0.

Huu ukawa ushindi wao wa sita mfululizo tangu walipopoteza mbele ya Manchester United, Desemba mwaka jana na kuweka rekodi ya kufungwa mechi 2 tu kati ya 21 walizocheza mpaka sasa.

Harry Kane yuko kwenye kiwango bora hivi sasa, akifunga mabao matatu dhidi ya West Brom. Kiungo Dele Alli amefunga mabao 7 kwenye mechi 5 alizocheza na kuifanya safu ya ushambuliaji ya Spurs kuwa moto wa kuotea mbali.

Kiwango chao msimu huu ni tofauti kidogo na msimu uliopita, wanaonekana kuimarika katika kila idara na ni wazi wana nguvu ya kubeba na kugombea taji msimu huu.

Kitu pekee anachotakiwa kuomba Pochettino ni kunusurika na mkosi wa majeruhi hasa kwa beki wake Jan Vertonghen, anayesumbuliwa na matatizo ya enka.

Mchezo ujao dhidi ya Manchester City utatupa picha kamili ya ubora wao msimu huu.

Lengo: Bado wana nafasi ya kubeba taji na kumaliza ndani ya Top 4.

Liverpool – Nafasi ya 3

Kiwango chao: Wamefungwa mara moja tu kwenye michezo 19.

Ratiba: Januari 21 – Swansea (nyumbani), Januari 31 – Chelsea (nyumbani), Februari 4 – Hull (ugenini).

Liverpool watakuwa wakijilaumu sana kwa kuruhusu bao la jioni walipocheza na Manchester United, kama wangebeba pointi 3 pale Old Trafford, wangekuwa kwenye nafasi nzuri sana ya kuishusha Chelsea kileleni.

Lakini pamoja na hilo, Liverpool walikuwa bora sana uwanjani licha ya kuwakosa nyota wao baadhi akiwamo Nathaniel Clyne, Joel Matip na Sadio Mane.

Pia waliweza kumtumia kwa mara ya kwanza kiungo fundi, Mbrazil Phillipe Coutinho, aliyerejea baada ya kupona majeraha yake.

Kocha wao, Jurgen Klopp, anaamini kikosi chake kilikuwa na nafasi kubwa ya kushinda dhidi ya Manchester United kama wangezidisha umakini kidogo tu wa kumkaba Zlatan Ibrahimovic.

Lengo: Wako kwenye mbio za ubingwa, lakini wazo kuu kwa sasa linaweza kuwa ni ‘Top 4’.

Arsenal – Nafasi ya 4

Kiwango chao: Hawajafungwa mechi 4 mfululizo.

Ratiba: Januari 22 – Burnley (nyumbani), Januari 31 – Watford (nyumbani), Februari 4 – Chelsea (ugenini).

Ushindi wa bao 4-0 walioupata dhidi ya Swansea ulikuwa na maana kubwa baada ya wapinzani wao, Manchester City, kupokea kichapo kama hicho katika dimba la Goodson Park dhidi ya Everton.

Baada ya pambano lile, kocha wao, Mfaransa Arsene Wenger, aliwataka vijana wake kuendelea na moto huu wa kugombea taji mpaka mwisho wa msimu.

Je, ni kweli Arsenal wana nguvu ya kubeba taji msimu huu? Ni mapema kuwaondoa lakini pia ni ngumu kukubaliana nao kutokana na ubora wa timu zilizo juu yao.

Lengo: ‘Top 4’, lakini bado wana nafasi ya ubingwa.

Manchester City – Nafasi ya 5

Kiwango chao: Wamefungwa michezo 2 kati ya mitatu waliyocheza hivi karibuni.

Ratiba: Januari 21 – Tottenham (nyumbani), Februari 1 – West Ham (ugenini), Februari 5 – Swansea (nyumbani).

Baada ya kichapo cha bao 4-0 walichokipata mbele ya Everton, kocha wa Manchester City, Pep Guardiola alijiondoa rasmi kwenye mbio za ubingwa wa EPL msimu huu.

Malengo ya City kwa sasa ni kuhakikisha wanamaliza ndani ya ‘Top 4’, kwa kikosi chao ni ngumu mno kuwaona wakiingia kwenye mbio za ubingwa msimu huu.

Kipa wao, Claudio Bravo amekuwa na makosa mengi yanayoigharimu City kupoteza pointi kwenye mechi nyingi za hivi karibuni na kuwaweka kwenye hatari ya kukosa michuano ya ligi ya mabingwa msimu ujao.

Kama Guardiola akirekebisha baadhi ya makosa kwenye kikosi chake hasa katika safu ya ulinzi, wana nafasi ya kuingia ndani ya ‘Top 4’, lakini kama wakibaki kama walivyo hivi sasa, hali itazidi kuwa mbaya zaidi kwao.

Lengo: Wasahau ubingwa, lengo ni ‘Top 4’.

Manchester United: Nafasi ya 6

Kiwango chao: Hawajafungwa kwenye mechi 12 mfulizo mpaka sasa.

Ratiba: Januari 21 – Stoke (ugenini), Februari 1 – Hull (nyumbani), Februari 5 – Leicester (ugenini).

Manchester United wanaonekana kuiamarika sana kipindi hiki na kucheza soka la nguvu japo ni muda mrefu hawajaingia kwenye nafasi 4 za juu.

Mpaka sasa wamefanikiwa kupunguza pointi kati yao na Tottenham, lakini wameachwa kwa pointi 12 na vinara wa ligi, Chelsea.

United hawana sababu ya kutafuta mchawi kwanini hawabanduki kwenye nafasi ya sita. Awali walitoka sare kwenye michezo 7, mitano ikiwa katika uwanja wao wa nyumbani, hii ndio sababu iliyowafanya wawe na tofauti ya pointi nyingi na timu za juu.

Lengo: ‘Top 4’, ubingwa ni mlima mrefu sana kwao kuupanda.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here