SHARE

MADRID, Hispania

MICHUANO ya Ligi ya Mabingwa Ulaya inatarajiwa kuendelea leo baada ya michezo miwili ya hatua ya 16 bora kuchezwa jana, huku Atletico Madrid wakiwa wenyeji wa Liverpool na Borussia Dortmund waliwakaribisha PSG.

Leo, michezo mingine miwili inatarajiwa kuchezwa. Atalanta watakuwa katika Uwanja wa San Siro wakiwakaribisha Valencia, kisha Jose Mourinho atakiongoza kikosi chake dhidi ya RB Leipzig ndani ya Uwanja wa Tottenham Hotspurs.

Mabao mengi ya michuano hiyo mikubwa Ulaya hufungwa katika hatua ya makundi, ndio maana kuna timu zaidi ya 10 zilizofanikiwa kuziona nyavu za wapinzani wao zaidi ya mara 200.

12.  Liverpool

MABAO: 207

MECHI: 120

Kabla ya kucheza jana na Atletico Madrid, Liverpool walifikisha idadi ya mabao 207 walipocheza dhidi ya mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu Hispania, La Liga.

Wanaweza kuongeza idadi ya mabao au wakabaki hapo hapo, sababu jana usiku walitarajiwa kucheza dhidi ya Atletico katika Uwanja wa Wanda Metropolitano.

11. Paris Saint-Germain

MABAO: 210

MECHI: 104

​Wakali wa nchini Ufaransa nao wanaingia kwenye orodha hii baada ya kufanikiwa kuonesha kiwango kizuri na kufunga mabao mengi. Jana walikuwa wageni wa Borussia Dortmund katika Uwanja wa Signal Iduna Park.

Baada ya kutolewa na Manchester United katika hatua ya 16 bora msimu uliopita, Thomas Tuchel alisema anataka kuona kikosi chake kikifanya vizuri msimu huu, ikiwezekana kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, kwa maana hiyo tutarajie kuona wakifunga mabao mengi.

10. Olympique Lyon

MABAO: 210

MECHI: 132

Olympique Lyon wanaweza wasitajwe kama timu kubwa Ulaya, lakini wameonesha kuwa wanaweza kuifanya kazi hiyo kwa umakini zaidi, ikiwa ni klabu ambayo imefunga mabao mengi zaidi kutoka Ufaransa, sawa na PSG. 

Safu ya ushambuliaji ya klabu hiyo sasa inaongozwa na Memphis Depay na Moussa Dembele, wote wamethibitisha kuwa na nguvu na uwezo wa kuisaidia Lyon kufikisha idadi mabao zaidi ya 200.

9. AC Milan

MABAO: 231

MECHI: 165

Wakiwa na mataji saba ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, AC Milan ni moja ya timu zenye mafanikio katika michuano hiyo, ingawa, hivi karibuni wamekuwa na mwenendo mbovu, mara ya mwisho kufika hatua ya robo fainali ilikuwa mwaka 2007 na kufanikiwa kutinga fainali kwa kuinyuka Liverpool.

Wakati huo walikuwa na washambuliaji wakali kama Filippo Inzaghi na Andriy Shevchenko ambao walifanikiwa kufunga mabao mengi na kuisaidia AC Milan kufikisha mabao zaidi ya 230.

8. FC Porto

FC Porto players lift the UEFA Champions League Trophy

MABAO: 253

MECHI: 188

Mabingwa wa taji hilo msimu wa 2003/04 dhidi ya AS Monaco, wakati huo wakifundishwa na Jose Mourinho, utabaki kuwa msimu wa kukumbukwa zaidi ndani ya klabu hiyo kutoka Ureno.

Msimu ule, Porto walifunga mabao 20 lakini waliendelea kuonyesha uwezo wao kwa miaka mingi, kwani mpaka sasa wamefunga mabao zaidi ya 250.

7. Chelsea

MABAO: 277

MECHI: 162

Chelsea walijitambulisha na kuwa wakubwa katika soka la Ulaya baada ya tajiri Roman Abramovich kuichukua klabu hiyo mwaka 2003. Miaka tisa baadae, walifanikiwa kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kuwachapa Bayern Munich.

Kocha wa sasa wa Chelsea, Frank Lampard alifanikiwa kufunga mabao 23 katika michuano hiyo, nyuma ya Didier Drogba aliyefunga mabao 36. Timu hiyo kutoka England imefunga mabao zaidi ya 270 tangu washiriki kwa mara ya kwanza.

6. Arsenal

MABAO: 281

MECHI: 177

​Mashabiki wa Arsenal hawajashuhudia kikosi chao kikicheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya tangu msimu 2016/17, awali walifanikiwa kutinga katika michuano hiyo kwa misimu 20 mfululizo wakiongozwa na Arsene Wenger.

Wana mambo mazuri ya kukumbukwa, walifika fainali mwaka 2006 na kufungwa na Barcelona, pia, Thierry Henry alifunga bao lililoipa ushindi dhidi ya Real Madrid ndani ya Uwanja wa Santiago Bernabeu, na kuwa timu ya kwanza ya England kushinda kwenye uwanja huo.

Lakini mpaka sasa, Washika bunduki wana hesabu mabao 281, kama wakirejea kwenye michuano hiyo, watahitaji kutafuta idadi ya mabao 300 ili kuonesha ukongwe wao.

5. Juventus

MABAO: 304

MECHI: 196

Mabingwa mara mbili wa taji hilo la Ulaya, pia, ni mabingwa wa Ligi Kuu Italia kwa misimu nane mfululizo na kutawala soka la nchini humo.

Mfungaji bora wa muda wote wa michuano hiyo, Cristiano Ronaldo yupo ndani ya kikosi hicho, japokuwa, wana kazi kubwa ya kuipiku Manchester United ambao wapo nafasi ya nne.

4. Manchester United

MABAO: 373

MECHI: 224

Tangu Sir Alex Ferguson aondoke ndani ya klabu hiyo mwaka 2013, Manchester United wanapitia katika kipindi kigumu, ikiwa msimu huu wanashiriki michuano ya Europa.

Mashetani wekundu hao bado wanasalia kuwa moja ya klabu kubwa duniani, na si rahisi kuweza kuona timu ikifanikiwa kufanya kama walivyofanya wao katika michuano hiyo.

Mwaka 1999 na 2008 walishinda mataji ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, shukrani kwa mashujaa wao kutoka Teddy Sheringham, Ole Gunnar Solskjaer mpaka kwa Edwin van der Sar, watakumbukwa ndani ya klabu hiyo.

Kama ilivyo kwa Arsenal, nao wanahitaji kufanya kazi kubwa ya kurejea katika michuano hiyo mikubwa ya Ulaya kwa ngazi ya klabu.

3. Bayern München

MABAO: 481

MECHI: 247

Kuna timu chache duniani zilizofanikiwa kuwatawala mabingwa wa Bundesliga, Bayern Munich.

Wababe hao wa Ujerumani licha ya kupata upinzani mkubwa kutoka kwa Borussia Dortmund, bado wapo katika ubora mkubwa na kuwa moja ya timu bora duniani.

Sasa safu yao ya ushambuliaji inaongozwa na Robert Lewandowski, wamebakisha mabao 19 kufikisha 500 katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

2. Barcelona 

MABAO: 511

MECHI: 254

Barcelona wamefanikiwa kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mara nne tangu Lionel Messi ajiunge nao mwaka 2004, na klabu hiyo kuwa moja ya timu zenye mafanikio.

Lakini misimu mitatu ya karibuni, Barcelona wameshindwa kufanya vizuri huku mafanikio yakiwa kutolewa katika hatua ya nusu fainali msimu uliopita, hata hivyo, ni klabu ambayo imefunga mabao zaidi ya 500.

1. Real Madrid 

MABAO: 565

MECHI: 265

Haishangazi kuona Real Madrid ni vinara wa kupachika mabao katika orodha hii, sababu ni klabu ambayo imetwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mara nyingi zaidi. Wamefanya hivyo mara 13.

Kabla Ronaldo hajajiunga na Juventus, wababe hao wa Hispania walikuwa moto wa kuotea mbali, kwani nyota huyo wa Ureno alifunga mabao 105, pia, wapo akina Raul Gonzalez na wengine wengi.

*Rekodi hizo kabla ya michezo ya hatua ya 16 msimu huu kuchezwa

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here