SHARE

NA EZEKIEL TENDWA,

ACHANA kwanza na habari hii ya Real Madrid kukabiliwa na kibarua kigumu cha kucheza na Bayern Munich Ligi ya Mabingwa Ulaya na badala yake piga picha ya namna mashabiki wa Chelsea wanavyokosa usingizi baada ya kusikia taarifa za Eden Hazard kutakiwa na Real Madrid.

Hapa hakuna namna, ni lazima watu wa Chelsea presha iwe juu kwani siku zote Madrid wanapotaka kumsajili mchezaji yeyote ni vigumu sana wanaommiliki kumzuia kwani kikosi hicho kina ushawishi mkubwa na fedha za kutosha.

Taarifa zilizopo ni kwamba, Madrid wameshaanza mikakati kabambe ya kumnyakua Hazard ambaye kwa sasa ni moja ya wachezaji tegemeo. Jambo kubwa linalotajwa ni mazungumzo ya awali yamefanyika na tayari pande zote mbili zinaelekea kukubaliana na kinachosubiriwa ni Chelsea kutaja dau lao.

Ni ukweli uliowazi kuwa, Real Madrid ni moja ya klabu ambazo ni ngumu sana kuzizuia zinapomhitaji mchezaji yeyote sasa mashabiki wa Chelsea, wanapokuwa na presha hilo si jambo la kushangaza kabisa na kinachosubiriwa ni kwamba muda ndio utazungumza.

Wakati presha ikizidi kupanda kwa mashabiki wa Chelsea, huku kwa Manchester United hali bado haijatulia kwani wanahisi siku za kipa wao, David de Gea, zinahesabika na Real Madrid ndio wanaoendelea kutajwa kuwavuruga Mashetani hao Wekundu.

Hii si mara ya kwanza Madrid kutajwa kumtaka De Gea na sasa presha ndiyo imezidi kuwa kubwa ambapo kwa vyovyote Mhispania huyo anaweza akaachana na timu yake hiyo na kuamua kurudi nchini kwao kujiunga na kikosi hicho kinachonolewa na Mfaransa, Zinedine Zidane.

De Gea ni moja ya makipa wenye uwezo mkubwa barani Ulaya kama ilivyo kwa Hazard alivyo na jina kubwa kutokana na kipaji chake akiwasulubu vilivyo mabeki wa timu pinzani ambapo sasa kinachosubiriwa ni ligi imalizike wenye wachezaji wao wajue kama wataendelea kubaki nao au wataondoka.

Wakati Madrid wakitia presha huko kwa Chelsea na Manchester United, wenyewe wanaugulia maumivu kimya kimya baada ya kupangwa kucheza na Bayern Munich Ligi ya Mabingwa barani Ulaya.

Hakuna timu iliyokuwa ikitaka kupangwa na Bayern Munich. Timu zote zinajua uwezo walionao Wajerumani hao, kila moja inajua kilichowatokea Arsenal ndiyo maana wasingependa kabisa kusikia wakiangukia kwenye mikono ya kikosi hicho kinachonolewa na Carlo Ancelotti.

Madrid ya Zidane ilikuwa radhi kupangwa na mahasimu wao Barcelona lakini si Bayern Munich. Walikuwa radhi kuangukia katika mikono ya Atletico Madrid lakini si Bayern, hata Barcelona wenyewe walinyoosha mikono juu na kumshukuru Mungu baada ya kupangwa na Juventus na kuepuka upanga huo wa Wajerumani.

Hata hivyo, kama Waswahili wanavyosema mwanamume lazima kujikaza, ndicho hicho ambacho kimetokea kwa kiungo wa Real Madrid, Toni Kroos ambaye amejitoa mhanga na kujitokeza waziwazi akisema kuwa hana presha na mchezo huo na kwamba lazima watawatupa nje wapinzani wao hao kwenye michuano hiyo.

Ni kweli kwamba, isingekuwa rahisi kwa mtu yeyote wa Real Madrid kujitokeza halafu aseme timu yao itafungwa, badala yake lazima aseme mchezo utakuwa mgumu lakini watapambana, ila kwa Kroos, yeye anachojua ni kwamba lazima wataibuka na ushindi, hiyo ikimaanisha kuwa mchezo huo kwake ni mwepesi tu.

Kroos ni mchezaji wa zamani wa Bayern Munich, anaijua timu hiyo ndani, nje kwani kabla ya kujiunga na Madrid alikuwa alitokea huko lakini kuurahisisha mchezo huo ni sawa ni ule msemo wa kujitekenya halafu ucheke mwenyewe. Ni kweli kwamba Madrid ni mabingwa watetezi, ni moja ya timu kubwa lakini mchezo dhidi ya wapinzani wao hao si wakubeza hata kidogo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here