SHARE

WAKATI wadau wa soka wakielekeza zaidi macho na masikio yao katika michuano mikubwa ya soka hapa nchini, Ligi Kuu Tanzania Bara, umefika wakati sasa wa kuelekeza hisia zetu katika michuano mingine ya Ligi Daraja la Kwanza.

Michuano hiyo imeanza rasmi jana, ikionyesha msisimko wa hali ya juu kiasi cha wadau walioanza kuishuhudia wanaishindanisha kwa karibu sana na michuano hii ya Ligi Kuu.

Miongoni mwa mambo yanayovutia ni ushindani ulioletwa na wachezaji mashuhuri waliowahi kucheza Ligi Kuu na hata timu ya Taifa na vilevile baadhi ya makocha walioamua kujikita huko kuanza kutafuta tiketi ya kucheza Ligi Kuu.

Mwaka huu michuano hiyo itazikutanisha timu 24 zitakazoumana kutafuta nafasi mbili za juu kupitia makundi matatu ya ligi ili ziweze kufuzu kucheza Ligi Kuu.

Baadhi ya timu zinazotajwa kuongeza hamasa katika michuano hiyo ni pamoja na Dodoma FC, inayonolewa na kocha mwenye mbwembwe, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, ambaye historia yake inawapa matumaini mashabiki wa timu hiyo kuelekea michuano ya Ligi Kuu.

Pia zipo timu kama KMC ya Kinondoni, Polisi Dar, Mufindi United,  Mlale JKT, POlisi Morogoro, Coastal Union, Mbeya Kwanza na nyingine ambazo kimsingi zimezidisha hamasa katika michuano hii mwaka huu.

Sisi DIMBA tunajua kwamba, macho na masikio ya wadau walio wengi na hata makocha pamoja na viongozi wa klabu za Ligi Kuu zimewekeza mawazo yao katika michuano hiyo inayoendelea.

Lakini sisi tunaona ipo haja ya kuigeukia michuano hii, kwa vile licha ya kuwa na msisimko, lakini ndiko kunakochezwa soka la hali ya juu lenye malengo ya timu na pia wachezaji mmojammoja.

Tumeona bila shaka kwamba hata benchi la ufundi linaloshiriki kutafuta vipaji kwa ajili ya kuteua timu ya Taifa, linaweza kupata vipaji vipya kutokea michuano hii, ambayo pia inahusisha wachezaji wengi chipukizi.

DIMBA tunazitakia kila la heri timu zote zinazoshiriki michuano hiyo, tunaamini italeta changamoto nyingine kwa soka la Tanzania, vilevile itatufikisha katika lengo letu la kuona tunapata timu imara ya taifa itakayotuletea mataji ya kimataifa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here