SHARE

NA MAREGES NYAMAKA

APRILI 6, 2019 ilikuwa ni mara ya kwanza Simba wanashindwa kuibuka na ushindi msimu huu kwenye ardhi ya nyumbani, Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam kwenye mchezo dhidi ya mabingwa mara tano wa Ligi ya Mabingwa Afrika, TP Mazembe.

Ilikuwa tofauti kabisa kuanzia hatua ya awali kilichowakuta Mbabane Swallows ya Eswatini na Nkana (Zambia) na  baadaye katika hatua ya makundi mbele ya JS Saoura(Algeria), Al Ahly(Misiri) pamoja na AS Vita (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Wote hawa walitunguliwa.

Sapraizi iliyofanywa na kocha wa Simba, Patrrick Aussems, katika mchezo wa TP Mazembe ni kumwanzisha benchi, Emmanuel Okwi, nafasi yake ikichukuliwa na Mrwanda, Haruna Niyonzima.

Kufanya vizuri kwa Niyonzima mchezo wa mwisho kufuzu hatua ya robo fainali dhidi ya AS Vita akitokea benchi, kulimshawishi Aussems?  Ni siri yake na benchi la ufundi, ingawa ukweli unaweza kubaki hivyo.

Dakika 90 hizo alizoaminiwa Niyonzima na kocha wake kwa mara ya kwanza tangu michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ianze, alizitendea haki kweli kweli mbele ya viungo wenye ubora mkubwa wa TP Mazembe.

Niyonzima alikuwa ni mchezaji pekee aliyegusa mpira mara nyingi zaidi (88), pasi nyingi kwenda kwa mlengwa akizifikisha kwa usahihi(58), huku akitengeneza nafasi tatu, lakini pia akikokota mpira kwa wastani mzuri, mara tano.

Kufikia hatua ya Claouts Chota Chama kufanyiwa mabadiliko, Niyonzima kumaliza dakika zote 90, uhalisia ni kwamba alikuwa bora akitimiza wajibu wake wa kuichezesha timu hasa kwenye kushambulia.

Niyonzima ambaye alianza kuitumikia Simba kwa kusuasua tangu msimu uliopita hadi miezi nane iliyopita, mechi mbili za mwisho dhidi ya AS Vita na TP Mazembe kuna kitu kikubwa cha kumfikirisha Aussems  sambamba na  mwekezaji, Mohamed Dewji ‘MO’.

Kivipi?  Kama walikuwa wamemwekea msitari mwekundu kwenye jina lake katika orodha ya wanaofunguliwa milango ya kutokea msimu ujao, basi sasa jina linawekewa nyota kuhamishiwa faili la wanaongezewa mikataba mipya.

Kwa staili yake ya uchezaji, uzoefu mkubwa hasa michuano mikubwa ya kimataifa katika nafasi anayocheza ya kiungo mshambuliaji, baada ya Chama anafuata yeye ingawa bado wanaweza kucheza sambamba kwa uweleano mkubwa.

Itakuwa makosa makubwa kumweka Niyonzima kapu moja na Mzamiru Yassini. Mbali na kipaji chake anajua kujipambanua kusoma alama za nyakati, lakini pia nidhamu ya mchezo wenyewe imekuwa msaada mkubwa kwake.

Dakika chache alizopata katika michezo mikubwa muhimu iko wazi, zimesahaulisha dakika 900 ambazo ni sawa na mechi alizokuwa akisugua benchi wakati mwingine jukwaani kabisa.

Tofauti yake na wachezaji wengine wengi nje ya uwanja ni namna alivyo na upeo mkubwa wa kujieleza, alichokifanya na matarajio yake mbeleni huku akiiunganisha timu ndani yake kama ilivyokuwa siku 14 zilizopita.

“Machi 16, 2019 ilikuwa ni siku kubwa sana katika maisha yangu ya kucheza soka ngazi ya klabu. Nimshukuru kocha (Patrick Aussems), kwa kuniamini na kunipa nafasi ya kucheza (dhidi ya AS Vita).

“Lakini dakika chache baada ya kuingia mchezoni nilipata maumivu makali kwenye kifundo cha mguu wangu. Niliamua kujikaza na kuendelea kucheza kwa sababu nilijiandaa kikamilifu katika mazoezi siku zote kwa ajili ya mechi kama hizi.

“Ndoto yangu tangu nikiwa mdogo ni kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo hakuna kitakachonizuia mimi kufika huko na sikutaka kuwaangusha mashabiki wa Simba SC Tanzania, mamilioni ya Watanzania na taifa langu la Rwanda.

“Niliamini kama roho yangu ni imara, basi maumivu ya mwili yasingeweza kuwa kikwazo kwangu. Hatimaye mapambano yetu yametufikisha robo fainali.

“Inshallah tutafika fainali kwa sababu tuna kikosi chenye uwezo wa kufanya hivyo na tuna mashabiki wasiochoka kuwa nyuma yetu.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here