SHARE
DOHA, QATAR - Saturday, December 21, 2019: Liverpool's captain Jordan Henderson bites his winners' medal after the FIFA Club World Cup Qatar 2019 Final match between CR Flamengo and Liverpool FC at the Khalifa Stadium. Liverpool won 1-0 after extra time. (Pic by David Rawcliffe/Propaganda)

MERSEYSIDE, England

BAADA ya dakika 90 kumalizika, kipyenga kilichokuwa kwenye mdomo wa mwamuzi, Damir Skomina kutoka Slovenia kilipulizwa kuashiria mwisho wa mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyowakutanisha Tottenham na Liverpool.

Wala hakukuwa na dakika 30 za nyongeza sababu shughuli ilimalizwa mapema na Liverpool baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 yaliyofungwa na Mohamed Salah na Divock Origi.

Medali za heshima zilivalishwa kwa wachezaji na benchi zima la ufundi la Tottenham, licha ya kupoteza mchezo huo kumbukumbu ilibaki imening’ing’inia kwenye shingo zao huku wakibubujikwa machozi yaliyoashiria kuumizwa.

Lakini Liverpool walipita mbele na kutunisha vifua mithiri ya mtu aliyepigwa ngumi ya mgongo, ilikuwa siku yao kufurahia baada ya kuisaka furahi hiyo kwa muda mrefu.

Wachezaji na benchi la ufundi wote walipita mbele kuvalishwa medali za ushindi kasoro mtu mmoja tu ambaye alibaki mwishoni, akisubiri kukabidhiwa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Alikuwa Jordan Henderson.

Inashtua kidogo kuona mtu ambaye hata baadhi ya mashabiki wa Liverpool waliamini hana uwezo wa kuvaa jezi ya timu hiyo ukitoa kupewa kitambaa cha unaondha.

Ndio, ni Henderson huyo ambaye alivaa kitambaa cha unahodha baada ya mkongwe wa Liverpool, Steven Gerrard kuamua kutimka ndani ya klabu hiyo aliyoitumikia kwa miaka zaidi ya 15.

Unadhani maisha ya kukataliwa yalianza Liverpool? Hapana, wala si kweli, kiujumla Henderson amekuwa akiishi hivyo.

Video moja iliyoangaliwa na watu zaidi ya milioni saba katika mitandao ya kijamii ilimwonyesha Henderson akiwa amemkumbatia baba yake huku machozi yakimtoka mithiri ya bomba lililokosa koki.

Nahodha alilia sana katika bega la baba yake, moja kwa moja ilitafsiriwa kuwa moyo wake ulikuwa umebeba siri nzito ya mafanikio yake aliyoyapata msimu huu akiwa na Liverpool.

Moyo wa Henderson ungekuwa unakubali mambo kwa urahisi pengine asingekuwa sehemu ya kikosi kilichotwaa ubingwa wa Ulaya baada ya miaka 14 kupita.

MKURUGENZI LIVERPOOL ATIMULIWA

Kwenye soka neno cha juu au 10% ni nadra sana kulisikia hasa huko barani Ulaya. Mwaka 2011 moja ya watu walioshutumiwa vikali na kuhusishwa na neno cha juu katika usajili alikuwa ni Damien Commoli wa Liverpool, je, unafahamu kwanini ilikuwa hivyo?

Mwaka huo, Commoli alipitisha usajili wa kiungo kinda, Jordan Henderson, kutoka Sunderland kwa ada ya pauni milioni 20 sawa na zaidi ya bilioni 41 za Kitanzania, ulikuwa ni usajili wa fedha nyingi sana aina ya mchezaji  kama Henderson.

Haikuishia kuwa maneno tu, kwani ugali wa Commoli ulimwagika mwaka mmoja baadaye alipotimuliwa kazi na ikawekwa wazi kwamba pamoja na mambo mengine usajili wa Henderson ukiwa sababu mojawapo ya kutimuliwa kwake. Unajua hii imekaaje? 

Ni kwamba Liverpool waliamini kwamba Commoli amewaingiza chaka katika usajili wa Henderson.

Pengine hivi sasa mabosi wa Liverpool wanakumbuka miaka saba iliyopita baada ya kumtimua Commoli, inawezekana waliwahi sana au ulikuwa wakati sahihi, maana wakati mwingine lazima mmoja atolewe kafara ili mwingine aishi kama mfalme.

RODGERS ALIMKATAA HENDERSON

Miaka saba imepita sasa tangu kocha wa zamani Liverpool, Brendan Rodgers alipomwita katika chumba chake cha hotelini na kumwambia kuwa hana mpango wa kuendelea kuwa na kiungo huyo raia wa England.

Unajua kichwa cha Rodgers kilikuwa kikiwaza nini? Basi iko hivi, alipanga kubadilisha na straika wa Fulham, Clint Dempsey ambaye hivi sasa amestaafu kucheza soka la kimataifa na kikosi chake cha Marekani.

Yaani timu ya Fulham ambayo ilipanda daraja na kushuka msimu huu ndio alitakiwa kuwa Henderson, mwisho wa siku machozi yaliyomwagika siku hiyo ilikuwa kama pale Madrid kwenye Uwanja wa Wanda Metropolitano.

Hiyo ilikuwa tiketi ya kwa heri kwa Henderson lakini aliamua kupambana ili Rodgers asiwe na mawazo hayo tena, alijituma kila kukicha kufuta kejeli za fedha nyingi zilizotumika kunasa saini yake kutoka Sunderland na kila kitu kilichosemwa.

Usiku mmoja aliketi na Gary Neville mchambuzi wa kituo cha Sky Sports na kumwambia kuwa “Hivyo ndivyo nimekuwa nikiishi tangu nikiwa mdogo, mara zote napenda kupambana, si kitu ambacho kinanifanya nijisikie vibaya ila hunijenga mara zote,” alisema Henderson.

Sasa amefanikiwa kupata zawadi ambayo imetokana na jsho lake lililovuja uwanjani kuwashawishi wote ambao walimkosoa na kumkataa, hivi sasa anapigiwa makofi huku sura zao zikiwa zinaangalia chini.

Mpaka sasa Henderson ameshacheza michezo 20 akiwa na kikosi cha timu ya Taifa ya England kinachoongozwa na Gareth Southgate.

KIGOGO LIVERPOOL AKUBALI

Kocha wa zamani wa Liverpool, Michael Beale alikaririwa akisema kuwa Henderson ni moja ya wachezaji muhimu ndani ya kikosi hicho baada ya kufanya kazi kubwa.

Wakati anasajiliwa kwa dau la pauni milioni 20, Beale alikuwa mmoja wa watu waliomshauri Commoli juu ya uwezo wa kijana huyo mdogo aliyekuwa akivaa jezi ya Sunderland.

“Mara zote kutakuwa na mtu mmoja kati ya milioni ambaye atakuwa na maendeleo bora au mazuri kuelekea kwenye kikosi cha kwanza lakini wachezaji kama Virgil van Dijk, Sadio Mane na Mohamed Salah wala hawakuhitaji muda kuingia kwenye mioyo ya mashabiki wa Liverpool.

“Namfahamu Henderson tangu akiwa Sunderland, ana sifa ya upambanaji hicho kilinivutia zaidi baada ya kumuona kwa mara ya kwanza katika mboni za macho yangu, wala haikuwa ngumu kutoa ushauri kwa Commoli.

“Tatizo kubwa ni kwamba alianza taratibu ndani ya kikosi cha Liverpool, alihitaji muda zaidi kuwa bora labda maneno ya mashabiki na wengine yamemfanya kuwa huyu shujaa wa sasa,” alisema Beale.

Huyo ndio Henderson ambaye inaaminika alikuwa sababu ya Liverpool kukosa taji la Ligi Kuu England msimu wa 2013/14 baada ya kukosekana katika michezo muhimu ambayo timu hiyo ilishindwa kupata ushindi.

Mashabiki wa Liverpool wanaliimba jina lake, wanamwimba kama shujaa baada ya Gerrard kuondoka ndani ya kikosi hicho, hiyo ni presha ambayo anakabiliana nayo kila siku.

Kila tatizo au kukataliwa kumemfanya awe shujaa, hakuamua kukacha safari ila alipita katika milima na mabonde ambayo yalimjenga kuwa mvumilivu zaidi.

Amekuwa nahodha wa aina yake, wakati Liverpool wanatinga fainali ya msimu uliopita kwa kuitoa AS Roma, Henderson alibeba bendera iliyoandika Sean Cox, shabiki ambaye alishambuliwa na wapinzani wao katika Uwanja wa Anfield kabla ya marudiano kwenye Mji wa Roma.

Ahadi yake kwa Sean Cox ilitimia msimu huu baada ya kushindikana uliopita.

Alicheza akiwa na maumivu katika mchezo wa pili wa nusu fainali dhidi ya Barcelona, lakini alikimbia kila mahali mpira ulipo kama nguruwe aliyekoswa na mshale kwenye mawindo.

Kila sekunde zilivyokuwa zikikimbia alionekana kuloa jasho kama alinyeshewa na mvua kubwa isiyokuwa na mwisho. Huyo ndiyo Henderson mnayemwona.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here