SHARE

MERSEYSIDE, England

ATLETICO Madrid watakuwa wageni wa vinara wa Ligi Kuu England, Liverpool katika Uwanja wa Anfield kwenye mchezo wa pili wa hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya ule wa kwanza Diego Simeone kuondoka kifua mbele kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Jurgen Klopp.

Simeone atakutana na moja ya timu bora duniani kwa sasa, huku Atletico Madrid wakiwa nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu Hispania, La Liga, nyuma ya Barcelona, Real Madrid, Sevilla FC na Getafe.

Liverpool ni timu imara msimu huu, lakini vipigo vitatu walivyopata msimu huu vimetoka katika michuano hii. Ilitokea katikati ya Septemba, mwaka jana walipofungwa na Napoli, wakati ambao timu hiyo ya Jurgen Klopp akiwa kileleni kwa tofauti ya pointi tano tu.

Pia, wakali hao wa England walifungwa mabao 3-0 na Watford katika mchezo wa Ligi Kuu England ikiwa ni kichapo cha kwanza kwao, kisha kukubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Chelsea kwenye mechi ya Kombe la FA.

Licha ya ubora walionao na kufanya vizuri katika Ligi Kuu England, mchezo wa leo dhidi ya Atletico Madrid ya Diego Simeone unatarajiwa kuwa mgumu kutokana na timu hizo mbili kucheza mpira wa nguvu na kasi, ukizingatia mechi ya kwanza iliyochezwa Hispania mwenyeji alipata ushindi.

HABARI ZA TIMU ZIKOJE?

Atletico walicheza michezo yao ya karibuni bila wachezaji wao nyota kutokana na kukumbwa na majeraha, watacheza dhidi ya Liverpool iliyokuwa na mastaa wao kwa asilimia kubwa.

Beki wa kulia wa Atletico, Kieran Trippier ataukosa mchezo wa leo sababu ya majeraha ya nyama za paja, tayari mchezaji huyo raia wa England amekosa mechi sita zilizopita.

Mshambuliaji Joao Felix ambaye alisajiliwa kwa pauni milioni 113 msimu huu, anatarajia kuwa sehemu ya kikosi cha Simeone, huku hivi karibuni aliwakaribisha mastraika wake tegemeo, Alvaro Morata na Diego Costa waliokuwa nje kwa majeraha.

Akiwa mshambuliaji alyefunga robo ya mabao ya Atletico msimu huu, uwepo wa Morata katika kuiongoza safu hiyo ya ushambuliaji litakuwa jambo muhimu kwa timu hiyo ya Hispania dhidi ya vijana wa Klopp.

Liverpool wana wachezaji wawili ambao wapo nje kwa muda mrefu, Nathaniel Clyne na Xherdan Shaqiri, huku Klopp akitarajia kumkaribisha kikosini nahodha wake Jordan Henderson.

Pia, kwa upande mwingine watakosa huduma ya kipa wa tegemeo raia wa Brazil, Alisson Becker ambaye alipata majeraha ya nyama za paja mazoezini.

REKODI ZAO ZIKOJE?

Timu hizo zimekutana mara tano katika michuano ya Ulaya, mara ya mwisho ilikuwa msimu wa 2009/10 kwenye nusu fainali ya Ligi ya Europa na Atletico walishinda kwa mabao ya ugenini baada ya sare ya mabao 2-2.

Kwa mara ya kwanza zilikutana katika hatua ya makundi msimu wa 2008/09, na mchezo kumalizika kwa sare ya bao 1-1. Ndani ya mechi hizo tano walizokutana, Liverpool ameshinda mara moja, huku wakienda sare mbili na Atletico Madrid wakishinda mara mbili.

Hata hivyo, Uwanja wa Anfield utakuwa na kumbukumbu nzuri kwa Liverpool ambao walipindua meza kwa kuifunga mabao 4-0 Barcelona msimu uliopita baada ya kuchapwa mabao 3-0 mchezo wa kwanza uliochezwa Nou Camp, msimu uliopita.

VIWANGO VYA SASA

Simeone hana rekodi nzuri kipindi cha karibuni, Atletico wameshinda michezo mitatu tu kati ya tisa waliyocheza katika mechi za La Liga na Spanish Cup ambako waliondoshwa na timu ya Daraja la Tatu, Cultural Leonesa.

Licha ya matokeo hayo mabaya kwenye ligi wapo nafasi ya tano, wameachwa mbali na timu mbili za juu Real Madrid na Barcelona ambao wanakimbizana kwenye mbio za ubingwa huku Atletico wakifanikiwa kupata pointi moja tu kwa vigogo hao katika michezo miwili waliyocheza.

Katika idara ya ulinzi wanaendelea kufanya vizuri, mabeki na kipa wao Jan Oblak wanafanya kazi na jitihada kubwa, isipokuwa kwenye safu ya ushambuliaji ambayo imelegalega na kuiangusha timu hiyo.

Kutoka michezo 27 waliyocheza msimu huu ya La Liga, wamefunga mabao 31 tu huku wakifungwa 21 na kuwa kati ya timu zilizoruhusu mabao machache msimu ndani ya Ligi Kuu, lakini idara ya ushambuliaji inayoongozwa na Morata wameshindwa kufanya kazi yao vizuri.

Leo, kama wakicheza na kufanikiwa kuwazuia Liverpool kufunga bao itakuwa faida kwao, kwani watakuwa salama na watafanikiwa kusonga mbele kwenye michuano hiyo.

Vinara hao wa Ligi Kuu England wapo imara katika idara ya ulinzi kwa wiki za karibuni, wamekuwa wakifanya vibaya, katika michezo minne iliyopita wameruhusu kufungwa mabao zaidi manne.

VIKOSI VITAKUAJE?

LIVERPOOL XI: ​Adrian; Alexander-Arnold, Gomez, Van Dijk, Robertson; Henderson, Fabinho, Wijnaldum; Salah, Firmino, Mané.

ATLETICO XI: ​ ​Oblak; Trippier, Savic, Felipe, Renan Lodi; Saul, Partey, Llorente, Koke; Felix, Morata.

TUTARAJIE NINI UFARANSA?

Borussia Dortmund watakuwa wageni wa wakali wa Ufaransa, PSG katika mchezo wa pili wa hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, mara baada ya kushinda mabao 2-1 ule wa kwanza katika Uwanja wa Signal Iduna Park.

PSG walisonga mbele baada ya kuwa vinara katika Kundi A lililokuwa na Real Madrid, huku Borussia Dortmund wakikatama nafasi ya pili kwenye Kundi F lililokuwa na Barcelona na Inter Milan.

Timu zote mbili zikiwa katika viwango vya juu kwenye michezo yao ya ligi, huku PSG akiwa na kazi kubwa ya kufanya ya kushinda ushindi wa mabao 2-0 ili kusonga mbele katika michuano ya Ulaya.

Kabla ya mchezo wa kwanza uliochezwa Ujerumani, timu hizo mara ya mwisho kukutana ilikuwa mwaka 2011, pia, mchezo wa leo utawakutanisha vijana wanaotabiriwa kufanya makubwa katika ulimwengu wa soka akina Jadon Sancho, Kylian Mbappe na Erling Haaland.

HABARI ZAO ZIKOJE?

Katika mchezo huo, inatarajiwa kwa PSG kumkaribisha Neymar ambaye alikosekana katika michezo ya hivi karibuni ya kikosi hicho kilichopo kileleni katika msimamo wa Ligi Kuu Ufaransa.

Itakumbukwa Neymar alikosa michezo mitatu ya hatua ya makundi msimu huu kutokana na kupewa adhabu kwa kuwatolea maneno ‘machafu’ waamuzi msimu uliopita.

Supastaa huyo raia wa Brazil bado hajaonesha kiwango kizuri katika michuano hiyo ya Ulaya msimu huu, amefunga mabao mawili kwenye michezo mitatu aliyocheza mpaka sasa.

Hata hivyo, kocha wa PSG, Thomas Tuchel bado hajathibitisha kama mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 atakuwa sehemu ya kikosi, kwani wamefanikiwa kufanya vizuri michezo minne ambayo Mbrazil huyo alikosekana, kwa kufunga mabao 17.

Dortmund wataendelea kukosa huduma ya nahodha wao, Marco Reus ambaye yupo nje kwa majeraha ya misuli huku akitarajiwa kurejea Machi, mwaka huu.

Emre Can ambaye alisajiliwa mwezi uliopita kutoka Juventus, amefanikiwa kuonesha kiwango kizuri katika michezo aliyocheza na kufanikiwa kufunga bao nzuri kwa shuti kali la mita 30 dhidi ya timu yake ya zamani, Bayer Leverkusen.

Mchezo huohuo, Dortmund walishuhudia kiungo wao Julian Brandt akipata majeraha ya enka, ingawa, bado haijathibitishwa kama utaikosa mechi ya leo dhidi ya PSG.

ZILIWAHI KUKUTANA?

Kabla ya mechi ya kwanza iliyochezwa Uwanja wa Signal Iduna Park, klabu hizo hazijakutana kwa miaka 10 sasa. Mwaka 2010, walicheza michezo miwili na yote kuisha kwa sare katika Kundi J la michuano ya Ligi ya Europa, lakini, PSG walifanikiwa kusonga mbele.

Straika Robert Lewandowski ambaye sasa ni kinara katika orodha ya wafungaji wa Ligi Kuu Ujerumani, Bundesliga akiwa na Bayern Munich, aliingia kutokea benchi kwenye mchezo wa mwisho uliochezwa Uwanja wa Parc des Princes, hata hivyo, alishindwa kuonesha cheche zake na mechi kuisha bila kufungana.

VIKOSI VITAKUWAJE?

PSG XI: ​ Navas; Kehrer, Silva, Kimpembe, Bernat; Gueye, Marquinhos, Paredes; Di Maria, Mbappe, Neymar.

Dortmund XI: Burki; Piszcek, Hummels, Zagadou; Hakimi, Can, Witsel, Guerreiro; Sancho, Haaland, Hazard.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here