SHARE

LEICESTER, England

TAKWIMU hazijawahi kudanganya na Jamie Vardy ndiye kinara wa kuwa na uwiano mzuri kati ya mashuti aliyojaribu na mabao aliyofunga kwenye orodha ya mastraika wenye mabao matano au zaidi ndani ya ligi tano kubwa Barani Ulaya.

Katika mashuti yote aliyojaribu kwenye lango la timu pinzani (kabla ya mchezo wa jana dhidi ya Norwich City) Vardy alikuwa amefunga mabao katika asilimia 39 ya mashuti aliyojaribu msimu huu.

Kwanini aonekane bora zaidi msimu huu? Ni kwa sababu ndani ya misimu miwili iliyopita Vardy alikuwa amefunga mabao katika asilimia 28.2 ya mashuti yake.

Lionel Messi amefunga katika asilimia 30.8 ya mashuti yake, Cirro Immobile ana asilimia 29.3, Wissam Ben Yedder (26.2%) na Robert Lewandowski (24.6%).

Makali yake hayo yameifanya Leicester ifanye vizuri msimu huu, lakini katika kuwekana sawa hebu twende pamoja katika uchambuzi huu. 

Vardy vs mastraika wakubwa Ulaya

Kwa sasa ndiye kinara wa mabao EPL akiwa amecheka na nyavu mara 16 yakiwemo mabao 11 katika mechi nane zilizopita akimpiku Tammy Abraham wa Chelsea kwa tofauti ya mabao matano.

Kiufupi Vardy ni straika namba mbili kwa kutupia mabao mengi ndani ya ligi tano kubwa Barani Ulaya akimfukuzia straika wa Lazio, Ciro Immobile mwenye mabao 17.

Kinara wa kucheka na nyavu mara nyingi katika kalenda ya mwaka huu ni Messi wa Barcelona akiwa na mabao 33 katika jumla ya mechi 29.

Wanaomfuatia Messi ni Vardy na ‘muuaji’ wa Bayern Munich, Lewandowski, ambao wote wana mabao 28 na Kylian Mbappe wa PSG anafuata akiwa ametikisa nyavu mara 27.

Vardy wa sasa na wa nyuma

Msimu huu Vardy amefunga mabao 16, ikiwa na maana kwamba anahitaji mabao mengine nane ndani ya mechi 22 ambazo ni nyingi iwapo akiepuka majeraha, lengo ni kuifikia idadi ya mabao 24 aliyofunga msimu wa ubingwa 2015-16.

Aidha Vardy wa sasa ana uwezo wa kufunga bao kila mechi (dakika 90) kwenye EPL. Msimu wa ubingwa alikuwa akifunga bao kwa kila dakika 131. 

Msimu huu anapiga mno mashuti yenye shabaha na kwa kila dakika 55 lazima afanye hivyo. Hata hivyo wastani wake wa kupiga mashuti umepungua kutoka kila dakika 35 ambao alikuwa nao msimu uliopita.

Lakini msimu wa ubingwa ndio alifanya vizuri zaidi katika eneo hilo kwa kujaribu shuti kwa kila dakika 27.

Hata hivyo, timu yake msimu huu haitegemei kupata pointi nyingi kupitia mabao yake. Kiufupi ule utegemezi uliokuwa umemzidi uzito umepungua kwa kiasi kikubwa na ndio chachu ya yeye kucheza kwa uhuru mkubwa.

Msimu huu amefunga mara 16 na amechangia pointi nane tu na wakati msimu wa 2015-16 kama sio mabao 15 aliyofunga kwenye mechi 16 za awali Leicester ingekusanya pungufu ya pointi 16.

Ameweza hata kuweka rekodi nyingine ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga bao katika mechi nane mfululizo za EPL tangu alipofanya hivyo mara 11 mwaka 2016. 

Vardy wa sasa ni tofauti?

Tulitegemea kumuona Vardy akipungua makali kutokana na umri wake mkubwa, lakini ameendelea kuwa wa moto. Nini sababu?

Brendan Rodgers ndiye sababu. Kocha wake huyo mpya ametengeneza mfumo na maelekezo mapya kwa Vardy kuwa hatakiwi kutumia nguvu nyingi kuwasumbua mabeki wanapokuwa na mpira.

Jukumu kubwa alilonalo Vardy wa Rodgers ni kufanya mikimbio katika sehemu muhimu zaidi ili aweze kufunga mabao. 

Kocha wake anaamini kwamba katika mtazamo wa kiulinzi, Vardy hana ulazima wa kuwakaba mabeki wote wanne peke yake. Sio kwamba hawezi, anaweza mno na ndio aina ya soka analolipenda. Kuwanyima amani mabeki.

Rodgers anataka kuona Vardy akicheza kulingana na alipofikia. Wenzake ndio wenye kazi kubwa ya kukaba na kumtengenezea nafasi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here