SHARE

NA SAADA SALIM

KAMATI ya utendaji ya Yanga inamsubiri kocha mkuu wa timu hiyo, Mwinyi Zahera, anayetarajiwa kutua nchini leo kutoka Ufaransa kwa ajili ya kuweka naye sawa mambo mbalimbali ikiwemo sakata la kipa Beno Kakolanya.

Zahera anatua leo kutoka Ufaransa alikokwenda kwaajili ya shughuli za kifamilia ambapo atakuwa na kikao na viongozi kabla kwenda jijini Mbeya kuungana na vijana wake wanaotarajia kucheza na Mbeya City Januari29, mchezo wa Ligi Kuu.

Yanga kwa sasa inaongoza ligi ikiwa na jumla ya pointi 47, huku Azam FC wakiwa nafasi ya pili kwa pointi 40 na Simba ikiwa nafasi ya tatu kwa pointi 30 huku akiwa na michezo minne mkononi.

Licha ya kuhitaji kuzungumzia mwenendo wa kikosi cha timu hiyo, lakini pia uongozi huo unahitaji kuweka sawa tofauti kati ya Zahera na kipa wao namba moja Kakolanya.

Kakolanya kwa sasa yupo njia panda kuweza kurejea kikosini mara baada ya kumalizana na uongozi wake kutokana na mgomo aliokuwa nao hivi karibuni ambapo kwa sasa suala limebakia kwa kocha Zahera kuweza kuamua juu ya kumrejesha baada ya kumkataa.

Taarifa za uhakika kutoka kwa kigogo ndani ya klabu hiyo ni kwamba, kwa sasa wanamsubiri Zahera arejee nchini na kukutana naye kwa ajili ya mazungumzo ikiwemo sakata la kipa huyo.

Alisema makipa waliokuwepo sasa wanafanya vizuri lakini umuhimu wa Kakolanya unaonekana ndani ya kikosi chao hasa atakapo umia mmoja wa makipa wao atabaki mmoja huku katika benchi akitegemewa kijana ambaye hana uzoefu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here