SHARE

KUANZIA juzi Jumatatu wagombea wa uchaguzi wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) walianza kufanya kampeni kwa ajili ya kushawishi wajumbe kuwapigia kura katika nafasi za uchaguzi utakaofanyika Agosti 12.

Kwa siku hizo tumeweza kuanza kusikiliza sera za wanasoka hao, ambapo wengi kati yao wamekuwa wakijitahidi kueleza dhima yao ya kutaka kulikwamua soka la Tanzania kutoka hapa lilipo na kulisogeza mbele.

Sisi DIMBA hatuna nia ya kurudia yale yaliyosemwa na wagombea hao wa nafasi mbalimbali na wala hatukusudii kunukuu kauli zao, kwani tukifanya hivyo tutakuwa tumejihusisha zaidi na kampeni hizo wakati nia yetu ni kutaka kuona tija kwa yale waliyonadi kuyafanyia kazi.

Ndiyo maana tumelazimika kuandika maoni haya tukiwaasa wagombea hao kufahamu uzito wa nafasi wanazoziona na pia mahitaji ya soka la nchi hii, ambalo kila uchao linazidi kurudi nyuma na kuwakatisha tamaa wapenzi wa mchezo huo.

Kutokana na hoja hizo na nyingine zenye mapungufu makubwa katika mustakabali wa mchezo huo, tumeona ipo haja ya kuwakumbusha viongozi hao wa baadaye wa TFF juu ya kuangalia kwanza jinsi Serikali ilivyoupa thamani mchezo huo kwa kujenga uwanja wa kisasa wenye miundombinu yote ya michezo ili waone umuhimu wa nafasi wanazozigombea.

Ni ukweli usiojificha kwamba soka letu lina changamoto nyingi kama vile kutokuwepo mikakati sahihi ya kukuza soka la vijana, kukosa viwanja vyenye hadhi kwa ajili ya ligi zetu na mambo mengine zaidi ya hayo.

Kwa maana hiyo kiongozi tunayemhitaji kwa ajili ya kutatua changamoto hizo si yule anayesimama majukwaani na kujisifia kwa usomi au uwezo jinsi anavyolijua soka la kimataifa, kwa kweli hayo hayana msaada wowote.

Tunawashauri wajumbe wa mkutano mkuu wa TFF ambao ndio waliobeba uwakilishi wa wapenzi wa soka la Tanzania, kufanya kazi ya hekima kwa kutuchagulia viongozi watakaopambana kutatua changamoto zilizopo.

Wengi wamepita na maneno matamu lakini matokeo yake tumeishia hapa tulipo, hivyo basi tufahamu wazi kwamba hakuna wakati wowote muhimu wa kuchambua mbivu na mbichi kwa kutumia jicho la ziada kama wakati huu.

Sisi DIMBA tunawatakia afya njema wagombea wote wanaoendelea na kampeni nasi tunaahidi kumuunga mkono mwanasoka yeyote atakayepewa dhima ya kuongoza nafasi mbalimbali zinazogombewa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here