SHARE

 

NA MARKUS MPANGALA

WAKATI fulani mwanazuoni Profesa William Edwards Deming ambaye alikuwa raia wa Marekani ambaye alifariki mwaka 1993 alipata kusema, “a bad system will beat a good person every time.”

Kwa tafsiri yangu isiyo rasmi: “Aghalabu mfumo mbaya unawaharibu watu au viongozi wazuri.” Lakini kwa wakati mwingine tunaweza kusema kinyume cha kauli hiyo, kwamba ‘watu/viongozi wabaya wanaweza kutumia mfumo mzuri au mbaya kutimiza ndoto zao.’

Mwanadamu anayo ndoto zake. Miongoni mwa ndoto za wanasiasa ni kushika madaraka ya ngazi za juu. Wapo wanasiasa ambao kwa namna moja au nyingine wanaweza kuanza ngazi za chini kama udiwani, kisha ubunge na urais.

Wapo wanasiasa ambao wanaanza moja kwa moja na ubunge bila udiwani kisha kuingia madaraka ya urais. Kuna wanasiasa wengine hawajawahi kuwa wabunge wala udiwani lakini moja kwa moja wanawania urais.

Kusema hivi sina maana kwamba wote lazima waanzie nafasi ya udiwani. Yumkini mwelekeo wa uongozi miongoni mwa wasomi wetu ni vema ungejikita kuanzia ngazi za serikali za Mitaa, ili kuepusha wapiga domo kuwa viongozi ambao hawana uwezo zaidi ya kelele zisizojenga taifa letu.

Kila mwaka wa uchaguzi mkuu wa udiwani, ubunge na urais. Watanzania wenzetu mbalimbali wamejitokeza kuwania urais. Nafasi ya urais ni ngazi ya juu na mwisho kabisa katika siasa. Yumkini kila mwanasiasa anaweza kuwa na istilahi za kila namna kwamba kashauriwa kugombea.

Hadi sasa kuna uvumi na waliojitangaza kuwania urais 2020 au 2025 na kadhalika. Bila kujali uwezo wa uongozi ukada wa chama chochote kile, ni vema kuhakikisha suala la afya za wagombea wa nafasi hiyo ni imara.

Kusema hivyo ni kwamba wagombea miongoni mwa wanasiasa wanaotajwa ni lazima tutambue afya zao kabla ya kuwakabidhi jukumu zito la kuongoza taifa letu. Tunafahamu kuwa Rais anakuwa na jopo la washauri na kuanzia suala la maisha ya kila siku akiwa kiongozi, siasa, utawala, uchumi, utamaduni, usalama na kazi.

Uzoefu unaonesha kuwa zipo nchi ambazo ziliingiza wagombea wagonjwa ambao wakafanikiwa kuchaguliwa kupata madaraka ya urais. Mwishowe wakadumu kwa muda mfupi sana kabla ya kumaliza vipindi vyao.

Mifano hiyo ipo katika nchi jirani ya Zambia, ambapo tangu kuondoka kwa Rais Frederick Chiluba imeshuhudia wanasiasa wenye afya zenye migogoro wakifanikiwa kushinda nafasi ya urais. Levy Mwanawasa alikuwa rais wa tatu wa Zambia. Katika rekodi za afya ya Mwanawasa inaonesha kuwa alipata ajali mwaka 1991 ambayo hadi alipokabidhiwa madaraka ya urais inaelezwa bado alikuwa dhaifu kiafya.

Mwanawasa alitawala Zambia kati ya mwaka 2002 hadi Agosti mwaka 2008 alipofariki dunia kwa ugonjwa wa kiharusi na presha. Katika kipindi chote cha kampeni za urais wa Zambia wapinzani wake walikuwa wakimshambulia kuwa hakuwa na afya bora. Waliamini Mwanawasa ni mgonjwa hivyo haikuwa sahihi kukabidhiwa madaraka ya urais.

Tuseme Mungu alifahamu mwisho wa Mwanawasa, lakini kibinadamu hali ilikuwa dhahiri asingemudu nafasi hiyo, hivyo walipaswa kumlinda. Wazambia wanatuletea mfano mwingine ambapo, walimpoteza Rais wao Michael Sata aliyeshinda nafasi hiyo dhidi ya Rupia Banda.

Banda alikaimu urais tangu kufariki kwa Mwanawasa, ndipo muda ulipomalizika akagombea moja kwa moja. Chaguo la Wazambia nalo lilianguka, na ilielezwa wazi kuwa Michael Sata maarufu kama ‘King Cobra’ afya yake ilikuwa tatizo.

Sata alichukua madara ya urais septemba 23, 2011 na kudumu hadi Oktoba 28, 2014. Kwa maana hiyo alidumu nafasi ya urais kwa kipindi cha miaka miwili na nusu tu. Baada ya kifo chake nafasi yake ilikaimiwa na Guy Scott.

Scott hakuweza kugombea urais kutokana na wazazi wake kuzaliwa Scotland, licha ya kuwa na uraia wa Zambia. Hata hivyo, katika kipindi cha kukaimu nafasi hiyo ilielezwa wazi kuwa Guy Scott hakuwa na afya bora, naye ilikuwa mgogoro kama bosi wake Sata.

Hii ina maana kuwa uteuzi unaofanywa na vyama vya siasa unapaswa kuliangalia kwa umakini sana suala la afya za makada wao wanaoomba nafasi za kugombea. Unyeti wa suala hili unasaidia kuepusha matatizo yanayoweza kuliathiri taifa kwa namna moja ama nyingine pamoja na wagombea wenyewe kusaidiwa kulinda afya zao kama haziwezi kumudu mikikimikiki.

Sina taaluma ya utabibu wala hila dhidi ya wagombea wowote kutoka vyama vya siasa, lakini tujihadhari sana na suala la afya ya mgombea yeyote wa urais, ubunge na udiwani.

Hii inatusaidia kujenga mfumo wa kujali afya za watu wetu na viongozi wetu. Inatuwezesha pia kuhakikisha kila mgombea anatumia njia salama kupata madaraka kuliko kumwachia yule aliye mgonjwa. Kwamba unapopuuza suala la afya za wagombea maana yake wanaweza kutumia udhaifu huo na kujipatia madaraka.

Mantiki yangu ni kwamba ili kuhakikisha taifa linakuwa na viongozi imara ni lazima tuzingatie suala la utimamu wa miili na akili zao. Ninapenda kuona nchi ikiwa na watu wenye afya njema huku wale walio wagonjwa tukiwawekea huduma za uhakika kukabiliana na magonjwa yao wawe na utimamu wa afya.

Tuwatumie watu wazuri kujenga mazingira bora ya kulinda afya za wagombea. Lakini pia tusitumie kigezo hicho kuwasulubu wale wasiostahiki. Hatujachelewa. Nje ya hapo tutakuwa watu wa misiba na matanga ya viongozi kama Zambia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here