SHARE
Gareth Bale

NA MAREGES NYAMAKA,

WAINGEREZA wawili, Jack Wilishere (Arsenal) na Joe Hart (Manchester City), ambao wametolewa kwa mikopo na klabu zao hizo, mwishoni mwa wiki walianza maisha mapya ya soka wakiwa na klabu mpya kwa rekodi tofauti.

Mastaa hao waliobahatika kupata nafasi ya kuingia kwenye vikosi vya timu zao  hizo, ilikuwa hivi ni Wilshere alianza vema kwa kuiwezesha Bournemouth kuibuka na ushindi wa 1-0 mbele ya West Brom.

Lakini upande wa pili kwa Hart anayekipiga Torino,  nyota yake ilififia mechi ya awali  baada ya timu yake hiyo kukubali kichapo ugenini cha bao  2-1 dhidi ya  Atlanta, licha ya kufanya kazi kubwa ya kupangua mashuti kadhaa langoni lakini Muingereza huyo mambo yalimdodea Sirie A.

Licha ya kuanza na rekodi mbaya ya kupoteza mchezo, Hart anatajwa kama mchezaji mahiri ambaye atafanya vizuri siku za usoni na kumfanya aingie kwenye orodha ya wachezaji  Waingereza waliowahi kunga’ra nje ya  ardhi ya England, Wales na Scotland.

Makala hii inakuletea orodha ya mastaa Waingreza  walionga’ra ligi mbalimbali duniani nje ya ardhi yao ya nyumbani, wakiwemo Charlie Phllippe, Alan Tyers na Gareth Bale.

Glenn Hoddle (AS Monaco)

Baada ya kuitumikia Tottenham kwa miaka 12, Hoddle alipata uhamisho wa kwenda Monaco ya Ufaransa  mwaka 1987. Msimu wake wa kwanza nyota huyo alionekana kuwa muhimu mahali hapo akiwezesha klabu hiyo kutwaa ubingwa wa ligi hiyo chini ya kocha, Arsene Wenger, ambapo Monaco ilikuwa haijatwaa taji hilo kwa muda wa miaka sita.

Na kumfanya Hoddle kutangazwa kama mchezaji bora wa mwaka wa kigeni katika Ligi ya Ufaransa, msimu uliofuata Muingereza huyo alifanikiwa kuingia wavuni mara 20 katika michuano yote aliyoshuka uwanjani.

Licha ya kuanza kusumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara, lakini aliisadia Monaco kwa mara nyingine kushinda Kombe la ligi mwaka 1991, kabla ya mkataba wake kumalizika na kuamua kurejea England katika klabu ya Swindon akitumika kama kocha mchezaji.

Gareth Bale (Real Madrid)

Bale aliipa kisogo Ligi Kuu England  majira ya kiangazi 2013, akijiunga  Real kwa kitita cha pauni milioni 85 akitokea Tottenham. Katika msimu wake wa kwanza tu, raia huyo wa Wales alifanikiwa kufunga jumla ya mabao 21.

Katika hayo mabao 21 yakiwemo yale yaliyowasaidia Real Madrid kuchukua taji la Copa del Rey, huku pia msimu huu akiingia kwenye orodha ya wachezaji watatu waliokuwa wakiwania tuzo ya mchezaji bora wa dunia.

Paul Lambert (Borussia Dortmund)

Lambert aliweka rekodi ya aina yake kama mchezaji  wa kigeni kutoka Scotland kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya akiichezea Borussia Dortmund mwaka 1997. Mscotland huyo ilikuwa ni miezi michache tu tangu asajiliwe na Dortumund akitokea  Motherwell mwaka 1996.

Mchezo huo wa fainali dhidi ya Juventus iliyokuwa na mchezaji matata Mfaransa, Zinedine Zidane, lakini Lambert alipata bahati ya kupenya kwenye kikosi cha kwanza cha Dortmund ambapo alifanikiwa  kutoa pasi ya mwisho kwa Karl-Heinz Riedle iliyozaa bao la kwanza katika ushindi wa bao 3-1.

Chris Waddle (Marseille)

Waddle hadi leo huwezi kukosa kwenye mafaili yake ya kumbukumbu kwenye kabati lake kutokana na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu Ufaransa maarufu kama Ligue 1,  mara tatu mfululizo ndani ya miaka mitatu katika klabu ya Marseille.

Marseille ambao walimnunua Waddle kwa pauni milioni 4.5 mwaka 1989, walimpandisha thamani nyota huyo ambaye pia alikuwa miongoni mwa mastaa kikosini kilichotwaa kombe la Europa mwaka 1991.

Steve McManaman (Real Madrid)

McManaman aliikacha Liverpool na kujiunga na Real Madrid mwaka 1999 akiwa kama mchezaji huru, msimu wake wa kwanza tu katika dimba la Santiago Bernabeu alifanikiwa kunyanyua kwapa baada ya timu yake Madrid kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi Valencia mchezo wa  fainali ya Ligi ya Mabingwa.

Na kuibuka shujaa wa mchezo kwani baada ya mchezo alikabidhiwa  tuzo ya nyota wa mchezo huo akitwaa tuzo binafsi ya nyota wa mchezo, baada ya miaka mitatu baadae Madrid wakashinda La Liga  mara mbili mfululizo na Ligi ya Mabingwa kwa mara nyingine ikiwa ni 2002, kabla mwaka uliofuata nyota huyo  kurejea ardhi ya nyumbani katika klabu ya Manchester City.

Gary Lineker (Barcelona na  Grampus Eight)

Lineker  alipata uhamisho wa majira ya kiangazi  kutua Barcelona kwa pesa kiduchu pauni milioni 2.7 akitokea Everton, ambapo katika maskani  mapya hapo msimu wake wa kwanza alifunga mabao 21 yakiwemo  ya EL Clasico, Barca wakiichakaza Real 3-2.

Ingawa mwaka huo timu iliambulia patupu wakikosa mataji yote msimu huo, lakini mwaka 1988, Lineker alinga’ara vilivyo ikiwemo mchezo wa mwisho wa Copa del Rey ambapo Barcelona ilinyakuwa taji hilo. Mwaka uliofuata alirejea England katika klabu ya  Tottenham Hotspur kabla ya kutimkia  Nagoya Grampus Eight ya Japan mwaka 1994.

Kevin Keegan (Hamburg)

Keegan ni nyota mwingine aliyeondoka Anflied mwaka 1977 na kutua Hamburg ya Ujerumani, hadi mwisho wa msimu wake wa kwanza alikuwa ameingia kimiani mara 12 na mwaka 1978 akapata  tuzo ya mchezaji bora wa kigeni.

John Charles (Juventus, Roma)

John Charles aliweka rekodi kipindi hicho mwaka 1957 kama mchezaji ghali kutoka Leeds United kwenda mahali hapo kwa  dau la pauni 65,000, msimu wa kwanza tu anapata tuzo ya mchezaji bora wa mwaka.

Wastani wake mkubwa klabuni hapo ulikuwa mkubwa, mwisho wa msimu akiwaokotesha makipa mipira nyavuni mara 28 na kuiwezesha Juventus kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu na Coppa Italia mara mbili. Soka lake la ushindani akalimazia Roma msimu wa mwaka 1962/63.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here