SHARE

MERSEYSIDE, England

WAKATI huu ambao tayari michezo mitatu ya Ligi Kuu England ikiwa imeshachezwa na klabu hiyo kufanikiwa kushinda michezo yote, makala haya yanakuletea wachezaji watano ambao wanatakiwa kumvutia au kumshawishi kocha wa timu hiyo Jurgen Klopp awaamini na kuwapa nafasi katika kikosi cha kwanza msimu huu.

Divock Origi

Divock Origi alipewa nyota ya ushujaa msimu uliopita, baada ya kufunga mabao muhimu akitokea benchi huku akionyesha kiwango cha kuvutia katika macho ya mashabiki wa Liverpool.

Tangu alipofunga bao muhimu dhidi ya mahasimu wao Everton, kisha kupachika mabao mawili muhimu kwenye nyavu za Barcelona katika mchezo wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ghafla upepo ulibadilika na kuwa kipenzi cha Klopp wakati kila alipohitaji matokeo ya ushindi.

Lakini ataweza kuwa mchezaji mwenye mwendelezo wa kuanza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza? Mchango wake aliouonesha msimu uliopita ulimfanya kuwa nyota muhimu.

Straika huyo mwenye umri wa miaka 24 anatakiwa kufanya kazi kubwa ili kuingia kikosi cha kwanza cha Liverpool chenye maskani yake Anfield.

Mkataba mpya wa muda mrefu aliosaini unaonyesha kuaminiwa na Klopp, kazi imebaki kwake kuthibitisha hilo kwa kufanya kazi kubwa ya kufunga mabao katika michezo ya kujiandaa na msimu ujao ili aanze kikosi cha kwanza.

Rhian Brewster

Bado hajafanikiwa kupata nafasi ya kucheza ndani ya kikosi cha Liverpool lakini anatajwa kuwa mmoja wa wachezaji chipukizi wenye vipaji vikubwa ndani ya timu ya mabingwa hao wa Ulaya. “Tumemwandalia nafasi muhimu msimu ujao,” alisema Klopp wakati wakijiandaa na msimu mpya.

Kocha huyo wa Ujerumani anamtaja Brewster kuwa ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa, straika huyo mwenye umri wa miaka 19 alikuwa sehemu ya wachezaji wa akiba katika mchezo wa fainali ya Ligi tya Mabingwa Ulaya dhidi ya Tottenham msimu uliopita.

Aliwahi kuwa mfungaji bora wa fainali za Kombe la Dunia chini ya umri wa miaka 17, alionyesha kuwa na jicho la goli katika umri mdogo, alifanikiwa kufunga mabao katika michezo ya kujiandaa na msimu mpya lakini bado hajafanikiwa kupata nafasi kikosi mpaka sasa kutokana na uwepo wa Sadio Mane, Roberto Firmino na Mohamed Salah katika idara ya ushambuliaji.

Adam Lallana

Baada ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Lallana alisema hana mpango wa kuondoka Liverpool, ataendelea kuwa hapo kwa msimu ujao huku akijiandaa na msimu wa 2019/20 kwa nguvu.

Ingawa, nyota huyo wa England mwenye umri wa miaka 31 anatakiwa kufanya kazi kubwa kumshawishi Klopp, baada ya kupata majeraha ya mara kwa mara ambayo yalimfanya kucheza michezo 16 tu kwa Liverpool na timu ya Taifa kwa kipindi cha miaka miwili, akiwa fiti ataweza kufanya kuishinda imani ya kocha wake?

Lallana ambaye mara ya mwisho alishiriki katika upatikanaji wa bao msimu wa 2016/17, alifunga mabao nane na kutoa asisti saba, lakini ghafla alishuka na kuishia kuwa mchezaji wa benchi, bado nafasi ipo ya kumfanya Klopp aamini kuwa mchezaji mwingine katika idara ya kiungo yupo.

Harry Wilson

“Mpango wangu ni kufanya kazi, nimerudi hapa sasa, imebaki kwangu kumshawishi kocha ili anipe nafasi katika kikosi,” Harry Wilson alifafanua baada ya kurejea Derby County alikokuwa anacheza kwa mkopo.

Mchezaji huyo raia wa Wales alifunga mabao 18 katika michuano yote msimu uliopita chini ya Frank Lampard, huku bao lake dhidi ya Manchester United likikumbukwa zaidi.

Wilson alisaini mkataba wa miaka mitano mwanzoni mwa msimu uliopita lakini mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 22, anatakiwa kufanya kazi ya kumshawishi Klopp ili apate nafasi ya kucheza msimu huu.

Ben Woodburn

Miaka miwili na nusu tangu Woodburn alipofanikiwa kuwa mchezaji mdogo zaidi katika historia ya Liverpool kufunga bao imekwisha. Sasa ana miaka 19, kinda huyo anatakiwa kufanya kazi kubwa msimu ujao.

Fowadi huyo alishindwa kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara msimu uliopita, wakati akicheza kwa mkopo katika kikosi cha Sheffield United na kurudishwa Liverpool mapema baada ya kuumia enka.

Klopp bado ana imani kubwa na kinda huyo akimtaja kuwa na kipaji, lakini kabla maamuzi ya kumtoa kwa mkopo kwa mara nyingine hayajafikiwa anatakiwa kupambana zaidi kumshawishi kocha wake ili abaki kikosini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here