SHARE

LONDON, England

KOCHA wa Arsenal, Arsene Wenger, ameanza kukumbushia sajili zake ambazo ‘zilikaribia’ kutimia, amemtaja Luis Suarez aisee! Mmoja wa wachezaji ambaye iwapo angetua Emirates huenda upepo huu mbaya unaoipitia ‘The Gunners’ ungekuwa unazungumziwa mdomoni tu.

Moja kati ya ishu zilizowahi kutikisa kwenye historia ya usajili ilikuwa ni hiyo ya Wenger kumtaka straika huyo wa zamani wa Liverpool.

Kocha huyo ameibuka na kuelezea vizuri jinsi mchakato huo ulivyokuwa, kuanzia mazungumzo na straika huyo anayekipiga Barcelona kwa sasa hadi kupeleka ofa yao pale Anfield.

Wenger alisema, Suarez ‘alikubali’ kujiunga na Arsenal, lakini kwa bahati mbaya ofa yao ya pauni milioni 40, huku thamani hiyo ikiongezewa pauni moja tu jambo lililomshangaza mmiliki wa Liverpool, John Henry.

Lakini ukweli wa ishu yenyewe alikuwa nao Wenger, ila hakutaka kuusema hapo awali na sasa ‘ameumwaga mchele’ kwa kusema Suarez alitaka kutua Arsenal kwani kila kitu kilikuwa kimeshakaa kwenye mstari, kilichobaki ni mshambuliaji huyo kupakia mabegi yake na kuelekea uwanja wa ndege.

Aidha, kwa msisitizo zaidi, Wenger alisema kama maelezo yake yanaonekana kutojitosheleza, atokee yeyote amuulize Suarez kama maneno hayo yana ukweli wowote.

“Suarez alikaribia kabisa kuja Arsenal. Kama klabu tayari tulifikia makubaliano. Ila tulishauriwa vibaya kwamba mkataba wake ulikuwa na kipengele cha kuvunja mkataba wake kwa thamani tuliyotajiwa, sambamba na kiwango cha mwisho. Kama mnaona maneno hayajitoshelezi muulizeni mwenyewe awape ukweli.

“Nina imani Suarez alitaka kujiunga nasi kabla Liverpool hawajamuuza. Waliamua kuendelea naye kwa mwaka mmoja zaidi, hivyo wakapata nafasi ya kuuboresha mkataba wake na kumwahidi wangemuuza nje ya England,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here