SHARE

NA SAADA SALIM


KAMA huipendi Yanga lakini unafuatilia mechi zake, ujue unajitafutia balaa la kupata presha!

Hivyo ndivyo walivyokuwa wakijinasibu mashabiki wa Yanga jana muda mfupi baada ya kumalizika kwa pambano la timu hiyo dhidi ya Lipuli FC na kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Huo ni mchezo wa tisa mfululizo kati ya 10, iliyocheza timu hiyo ikishinda yote na kutoka sare moja dhidi ya watani wao wa jadi Simba uliopigwa Uwanja wa Taifa.

Mchezo wa jana ulikuwa wa ushindani kwa timu zote kuanzia dakika ya kwanza ambapo wenyeji Yanga walionyesha nia ya kutaka bao la mapema.

Walifanikiwa kupata bao hilo dakika ya tisa likifungwa na Heritier Makambo kwa mguu wa kushoto baada ya kupokea krosi kutoka kwa Mrisho Ngassa akiwa ndani ya boxi la penalti.

Baada ya kupata bao hilo Yanga walionekana kutakata kwa kufika mara kwa mara katika lango la Lipuli, kupitia mchezaji wake Paul Godfrey dakika ya 22 na 25 lakini walinzi wa Lipuli walimnyima nafasi ya kupiga shuti au kutoa krosi.

Lipuli walikuwa imara katika safu ya ulinzi na walikuwa wakifanya mashambulizi ya kushutukiza na nusura Issa Rashid aipatie timu yake bao dakika ya 27 baada ya kupiga shuti na mpira kutoka nje kwa kupita pembeni ya lango la Yanga.

Katika kipindi cha pili, Lipuli walianza kwa kasi ambapo dakika ya 46, Paul Nonga alikosa nafasi ya wazi baada ya kupokea pasi kutoka kwa William Lucian lakini akashindwa kuutuliza na hatari hiyo kuokolewa na Thabani Kamusoka.

Katika mchezo huo ulioamuliwa na mwamuzi wa kati Abukabari Mturo kutoka Mtwara amempa kadi ya nyano, Novatus Lufunga baada ya kumfanyia madhambi Ngassa dakika ya 55.

Dakika ya 56, Seif Abdallah wa Lipili alipewa kadi ya njano kwa kumfanyia madhambi Gadiel Michael huku Kelvin Yondani naye pia akionyeshwa kadi ya njano dakika ya 73 kwa kumcheza rafu Issa Rashid.

Refa Mturo alilazimika kumtoa nje kwa kadi nyekundu beki wa Yanga wa kulia, kinda, Paul Godfrey, kwa kumchezea rafu mchezaji wa Lipuli FC.

Kutokana na upungufu huo wa wachezaji uwanjani na zikiwa zimesalia dakika nne mpira kumalizika, kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera, alimtoa Ngassa na nafasi yake kuchukuliwa na Juma Abdul lengo likiwa ni kuimarisha safu ya ulinzi.

Kwa ushindi huo muhimu, Yanga inapanda hadi nafasi ya pili ikiwa na pointi 25 ikizidiwa pointi mbili na vinara Azam FC huku wakiwashusha watani zao Simba ambao wamejikusanyia pointi 23.

Kikosi cha Yanga: Beno Kakolanya, Paul Godfrey, Gadiel Michael, Abdallah Shaibu `Ninja`, Kelvin Yondani, Feisal Abdallah `Fei Toto`, Mrisho Ngassa, Makka Edward,  Heritier Makambo Thaban Kamusoko /Said Makapu dakika 71 na Antony Matheo/ Deus Kaseke dakika 66.

Lipuli: Mohammed Yusuph, William Lucian, Ibrahim Job, Paul Ngalema, Novalty Lufunga, Miraji Adam, Jimmy Shoji/ Seif Abdallah dakika ya 33, Zawadi Mauya, Paul Nonga na Issa Rashid.

Katika mchezo mwingine wa ligi uliopigwa jana Uwanja wa CCM Kirumba, wenyeji Mbao FC walilazimika kutoka nyuma na kusawazisha mabao yote mawili dhidi Mbeya City.

Mbeya hadi wanaenda mapumziko walikuwa wakiongoza kwa bao moja lililofungwa na Iddy Selemani ‘Nado’ katika dakika ya 11 na dakika tatu kipindi cha pili, Eliud Ambokile alifunga bao la pili na safa amefikisha mabao nane katika mbio za kuwania Kiatu cha Dhahabu.

Mbao FC walicharuka dakika 10 za mwisho na kufanikiwa kupata bao la kwanza dakika ya 83 kupitia kwa Evarigester Mujwahukwi na lingine dakika ya 90 na yote akiyafunga kwa kichwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here