SHARE

NA MWANDISHI WETU,

YANGA watapokea kitita cha fedha leo kutoka kwa wadhamini wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom, baada ya kuibuka mabingwa msimu wa 2016/17.

Utoaji tuzo ya waliotia fora kwenye Ligi Kuu Bara msimu wa 2016/17 utafanyika leo katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Mshambuliaji wa Yanga, Simon Msuva, naye atapokea Sh milioni 5.8, kiasi ambacho pia kitapokelewa na mshambuliaji wa Ruvu Shooting, Abdulrahman Mussa, baada ya wachezaji wote wawili kuibuka wafungaji bora kila mmoja akifunga mabao 14.

Msuva pia yumo kwenye orodha ya wanaowania tuzo ya Mchezaji Bora pamoja na Aishi Manula (Azam), Shiza Kichuya (Simba), Haruna Niyonzima (Yanga) na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ (Simba).

Joseph Omog wa Simba, Mecky Mexime wa Kagera Sugar na Ettiene Ndayiragije wameteuliwa kuwania tuzo ya Kocha Bora wakati tuzo ya Kipa Bora inawaniwa na Owen Chaima (Mbeya City), Juma Kaseja (Kagera Sugar) na Manula (Azam).

Watakaowania tuzo ya Mchezaji Bora wa Kigeni ni Niyonzima (Yanga), Method Mwanjale (Simba) na Yusuph Ndikumana (Mbao), huku Shomari Lawi (Kigoma), Elly Sasii (Dar es Salaam) na Hance Mabena (Tanga) wakiteuliwa kuwania tuzo ya Mwamuzi Bora.

Tuzo ya Mchezaji Bora Anayechipukia inawaniwa na Mbaraka Yusuph (Kagera Sugar), Shaaban Idd (Azam) na Mohammed Issa (Mtibwa Sugar).

Katika kumuenzi aliyekuwa mchezaji wa timu ya Taifa ya vijana aliyefariki dunia akiwa uwanjani, imebuniwa Tuzo ya Ismail Khalfan hususan kwa mchezaji chini ya umri wa miaka 20 ambapo wanaowania msimu huu ni Shaaban Idd (Azam), Abdalah Masoud (Azam) na Mosses Kitambi (Simba).

Aidha, kutakuwepo na tuzo ya heshima, timu yenye nidhamu na kikosi bora cha msimu ambavyo vyote vitatangazwa leo ukumbini ikiwemo kuonyesha mabao 10 bora kabla ya kutangaza goli bora la msimu.

Katika hatua nyingine, kunazo tetesi uongozi wa Simba umegomea tuzo za leo kwa kile walichodai kutotambua ubingwa wa Yanga hadi pale Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) litakapojibu rufaa yao baada ya kupokwa pointi tatu katika mechi dhidi ya Kagera Sugar.

Simba walisusia medali ya mshindi wa pili baada ya mchezo wao wa mwisho dhidi ya Mwadui uliochezwa Jumamosi iliyopita katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here