SHARE

NA JESSCA NANGAWE

KIKOSI cha Yanga, leo kitakuwa ugenini kusaka pointi tatu dhidi ya wenyeji wao, Mtibwa Sugar, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Huu ni mchezo wa kisasi kwani Mtibwa Sugar itakuwa ikikumbuka kipigo cha bao 1-0 katika mzunguko wa kwanza, Februari 2 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es salaam.

Yanga inaingia uwanjani ikitoka kwenye majeraha ya kuambulia sare ya bao 1-1 na Mwadui FC katika mchezo uliochezwa Jumapili iliyopita Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ikiwa  nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo na jumla ya pointi 68 baada ya kucheza michezo 36; ikishinda 18, kutoka sare 14  na kupoteza nne, imebakiza michezo miwili ili kukamilisha michezo yake msimu huu.

Mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu Bara, wataingia kwenye mchezo huo wakihitaji pointi tatu ili kuendelea kujiimarisha katika nafasi ya pili ambayo pia inatolewa macho na Azam FC wanaotofautiana kwa pointi mbili tu.

Kocha mkuu wa Yanga, Luc Eymael, ameahidi kumaliza michezo iliyosalia kwa heshima, kwani anatambua licha ya kuondolewa kwenye ndoto zao, lakini wana sababu ya kumaliza ligi hiyo wakiwa nafasi ya pili.

Mtibwa Sugar nayo haitakuwa na mzaha katika mchezo huo kwani inashika nafasi ya 14 katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 41, baada ya kushuka dimbani mara 36; ikishinda 10, sare 11 na kupoteza 15.

Wakata Miwa hao watahitaji ushindi katika mchezo huo ili kuweka hai matumaini yao ya kubaki Ligi Kuu Bara msimu ujao.

Endapo Mtibwa Sugar itakubali kichapo katika mchezo huo, huku timu wanazolingana nazo pointi, Lipuli, Mwadui FC na Alliance FC zikishinda michezo yao, itazidi kujiweka pabaya hata kama itashinda mchezo wake wa mwisho.

Akizungumza kuelekea mchezo huo, Ofisa Habari wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru, alisema huo ni mchezo mgumu kwao ila watapambana kupata matokeo chanya ambayo yatawafanya wabaki ndani ya ligi.

“Tunacheza na Yanga, tunamtanguliza Mungu kwenye mchezo wetu, tutacheza kwa jitihada zote na nguvu zetu ili tupate ushindi kwani tupo katika hali mbaya na tukiwa tumesalia na michezo miwili,” alisema.

Mbali na mchezo huo, ligi hiyo itatimua vumbi katika viwanja vingine vinne, ambapo Mbao FC itakua nyumbani kuialika Namungo FC, mchezo utakaopigwa Uwanja CCM Kirumba jijini Mwanza.

Mbao FC iliyo nafasi ya 19 kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 39, italazimika kushinda mchezo huo ili kufufua matumaini ya kubaki kwenye ligi hiyo.

Mtanange mwingine utakuwa kati ya Singida United ambayo tayari imeshashuka daraja dhidi ya Kagera Sugar, Uwanja wa Liti Singida.

Mwadui FC ambayo haiko salama kwenye msimamo wa ligi ikishika nafasi ya 16 na pointi zake 41, itakuwa na kibarua kigumu cha kusaka pointi tatu muhimu mbele ya Biashara United, mchezo utakaopigwa Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga.

KMC itakuwa na shughuli pevu dhidi ya Tanzania Prisons, mchezo utakaorindima kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here