SHARE

NA EZEKIEL TENDWA

YANGA wameuchungulia msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wakagundua kuwa wapo nafasi ya tatu, na sasa wanaondoka kesho kuelekea Shinyanga kuwavaa Mwadui FC, huku wakiwa na kikosi cha maangamizi.

Kocha Mkuu wa mabingwa hao watetezi, Hans Pluijm, ameahidi kuendeleza ubabe na kukisambaratisha kikosi cha kocha mwenye maneno mengi, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, katika uwanja wao wa nyumbani uliopo Mwadui, Shinyanga.

Katika msimamo wa Ligi hiyo, Yanga wanashika nafasi ya tatu, wakiwa na pointi saba katika michezo yao mitatu waliyokwisha kucheza mpaka sasa, huku Azam na Simba zikikabana koo kileleni kila moja ikiwa na pointi 10, wao wakiwa wamecheza michezo minne.

Yanga wanaondoka kesho wakiwa na kauli moja tu ambayo kwa sasa imesambaa mitaani ya kusepa na kijiji, wakimaanisha kuwa itabidi mabeki wa Mwadui wajizatiti, kwani safu ya ushambuliaji inayoongozwa na Donald Ngoma na Amis Tambwe itakuwa na kasi ya ajabu.

Yanga itaingia katika mchezo huo ikiwa na hasira kali kutokana na kumbukumbu ya kutoka sare ya kufungana mabao 2-2 katika mchezo wa msimu uliopita, uliochezwa katika Uwanja wa Kambarage, mkoani humo.

Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit, ameliambia DIMBA Jumatano kuwa wachezaji wote wapo katika hali nzuri na wale waliokuwa wakizitumikia timu zao za Taifa, akiwamo Haruna Niyonzima na Vicent Bossou, wameshawasili na kuungana na wenzao tayari kwa kutafuta pointi tatu muhimu.

“Niseme tu kwa upande wetu kama uongozi kila kitu kipo sawa, japo siwezi kusema kwamba tunaondoka lini, wachezaji wote wapo katika hali nzuri na benchi letu la ufundi linafanya kazi yao ipasavyo,” alisema.

Akizungumzia mchezo huo, alisema licha ya changamoto zinazowakabili, ikiwamo uchovu wa wachezaji baada ya kutumika kwa muda mrefu, hasa kwenye michuano ya kimataifa iliyokuwa ikiwakabili, watahakikisha wanaondoka na pointi tatu.

“Kuna changamoto nyingi, kwani kama unavyojua wachezaji wetu walitumika sana, ila yote kwa yote Yanga ni timu kubwa na kila tutakapofika tutaondoka na pointi tatu,” alisema.

Katika mchezo huo, Yanga itawategemea sana washambuliaji wake Donald Ngoma, Amis Tambwe ambaye ni mfungaji bora wa msimu uliopita pamoja na Obrey Chirwa, ambao wanatarajiwa kuwakimbiza vilivyo mabeki wa Mwadui FC.

Kwa upande wa safu ya ulinzi, Vicent Bossou anatarajiwa kuwaongoza wenzake kama alivyoiongoza timu yake ya Taifa ya Togo kutinga michuano ya AFCON, huku Thaban Kamusoko na Haruna Niyonzima wakitawala eneo la katikati.

Hata hivyo, wakati Yanga wakisema hayo, Kocha Mkuu wa Mwadui, Julio, ameyasikia maneno yao kisha akasema: “Sisi hatuogopi chochote, hao Yanga waje tu wanaiona shughuli yetu huku”.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here