SHARE

NA WINFRIDA MTOI

YANGA inatarajia kushuka dimbani leo kuvaana na Kagera Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania, huku nyota wapya wa timu hiyo wakitarajiwa kuwa sehemu kubwa ya kikosi kitakachoanza.

Mchezo huo utakaochezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, utakuwa ni mtihani wa kwanza wa kocha mpya wa timu hiyo, Luc Eymael aliyeanza kazi  ya kufundisha Jumapili iliyopita.

Eymael alichukua mikoba ya Mwinyi Zahera, aliyeachana na timu hiyo Novemba, mwaka jana na nafasi yake kukaimiwa na Charles Mkwasa tangu alipoondoka.

Mkwasa alikiongoza kikosi hicho katika mechi nane za Ligi Kuu na moja Kombe la Shirikisho Tanzania (ASFC).

Ukiachana na kocha mpya, watakaongaliwa zaidi ni wachezaji wapya wa timu hiyo ambao hawakupata muda wa kuonekana vizuri katika mechi zilizopita kutokana na muda waliosajiliwa.

Wachezaji ambao wameonekana na kuanza kukubalika ni na wapenzi wa Wanajangwani hao, ni Adeyum Saleh, Ditram Nchimbi na Tarig Seif, lakini wengine bado hawajaonyesha makali yao.

Nyota wanaosubiriwa kwa hamu kutokana na kucheza dakika chake katika mechi zilizopita, ni Yikpe Gnamien na Haruna Niyonzima.

Mchezo huo ambao unakuwa wa 13 kwa Yanga,  unatarajia kuwa na ushindani mkubwa kutokana  aina ya timu wanayokutana nayo na matokeo ya nyuma yaliyopatikana kwa vikosi vyote.

Wanajangwani hao wanashuka dimbani ikiwa mchezo uliopita wametoka sare ya mabao 2-2 na Simba, mechi iliyochezwa Januari 4, mwaka huu Uwanja wa Taifa.

Katika msimamo wa ligi hiyo, Yanga inashika nafasi ya saba ikiwa na pointi 25, ikishinda saba, sare nne na kupoteza mmoja.

Kwa upande wa Kagera Sugar itashuka  dimbani  ikiwa na hasira za kupoteza mechi tatu mfululizo, mara ya mwisho ikipokea  kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Polisi Tanzania  kwenye  Uwanja Ushirika Moshi, Kilimanjaro.

Akizingumzia mchezo huo, kocha wa Yanga, Eymael, alisema  amepata muda wa kuangalia video za wapinzani wake na atajipanga kulingana na mbinu  atakazotaka kutumia.

“Ni siku chache tangu nimekaa na timu, lakini kitu kizuri nimepata muda wa kuangalia  video za mechi zilizopita za Kagera Sugar, hakuna tatizo na wachezaji nimewaona wako vizuri,” alisema.

Kwa Upande wake, Kocha wa Kagera Sugar Meky Mexime alisema mchezo huo ni muhimu kwa kikosi chake kushinda ili kurudisha morali baada ya kushindwa kufanya vizuri katika michezo mitano iliyopita.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here