SHARE

NA WINFRIDA MTOI

KWA misimu miwili mfululizo, Yanga wamekuwa wanyonge mbele ya Simba, hasa baada ya kushindwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa kipindi hicho chote.

Wanajangwani hao walikuwa hawana ujasiri wa kujigamba mbele ya watani zao ambao wamekuwa wakionekana kuwa vizuri kila idara kuanzia uchumi hadi kikosi.

Kitendo cha Yanga kukosa fedha za kusajili wachezaji wazuri katika misimu miwili mfululizo, kimekuwa kikiwaumiza wapenzi wa timu hiyo kutokana na kejeli wanazopata kutoka kwa watani wao Simba.

Wanajangwani hao waliendelea kuvumilia  huku wakiweka mikakati yao na kuanza mwaka 2020 kwa kasi mpya.

Yanga ilifungua mwaka kwa kuzima ngebe za watani zao Simba, wakipindua meza dakika za mwisho wakitoka sare 2-2 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliopigwa Januari 4, Uwanja wa Taifa.

Mchezo huo uliifanya Yanga kubaini udhaifu wa mahasimu wao hao na kuendelea kufanya usajili wakuziba kila idara iliyokuwa na upungufu.

Simba imekuwa kikosi bora kutokana na wachezaji waliosajiliwa, ubora wa benchi la ufundi na uwekezaji waliofanya uliochangia kufika hadi robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika Msimu uliopita.

Sasa Yanga imesoma mchezo mzima, kwani wadhamini wao GSM wameamua kufanya kweli huku uongozi ukisimama kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa.

Wanajangwani hao walianza kushusha vifaa vya nguvu katika usajili wa dirisha dogo kwa kusajili washambuliaji watatu, beki na kiungo ambao wamekifanya kikosi hicho kubadilika.

Kama vile haitoshi  wakaingia katika kuboresha benchi la ufundi, ikishusha kocha Mbelgiji aliyetamba na timu mbalimbali Afrika, Luc Eymael.

Inafahamika kuwa kitu kingine kilichokuwa kinawapa jeuri Simba na kucheza mpira wa kasi bila wachezaji kuchoka ndani ya dakika 90, ni uwepo wa kocha wa viungo Adel Zrane.

Yanga nayo imejibu mapigo na kuleta kocha wa viungo kutoka Afrika Kusini, Riedoh Berdien, makocha wote tayari wameanza kazi ya kunoa kikosi hicho.

Unaambiwa mikakati yote hiyo ni kuhakikisha wanaipoteza Simba  kwa kuanza kuivua taji la Ligi Kuu  wanaloshikilia ili kutinga kimatifa kwa kishindo bila kutegemea kubebwa.

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, amethibitisha hilo kwa kusema wanafahamu kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu na kufanya vizuri kimataifa si kazi rahisi, ni lazima wajipange.

Mwakalebela aliliambia DIMBA Jumatano kuwa, wamebaini hakuna kitu kizuri kinachokuja bila kuingia gharama, wamemleta kocha mwenye viwango vya juu ili kufikia malengo.

“Yanga ni timu yenye historia ya nchi, hatutafanya makosa, tumejipanga msimu huu ubingwa unatua Jangwani, huyu kocha hatujamleta kwa kubahatisha, tunajua atafanya kile tunachohitaji,” alisema.

Katika tukio lingine unaloweza kusema la kimafia ni pale kocha Eymael alipoamua kuifuatilia Simba katika mechi zake mbili za Kombe la Mapinduzi dhidi ya Azam, hatua ya nusu fainali na Mtibwa ambayo iliitupilia nje.

Baada ya kuisoma, kocha huyo ameekeza kusikitishwa kwake na kuchelewa kuifahamu, vinginevyo wasingetoka katika mchezo ule wa ligi.

Hata hivyo ameahidi kuwafuta machozi mashabiki wa Yanga kwa kupata ushindi katika mechi zake mbalimbali pia kuwaadabisha Simba watakapokutana nao tena.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here