SHARE

NA CLARA ALPHONCE,

WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga, wameliomba Shirikisho la Soka  Barani Afrika (CAF), kuhamisha mchezo wao wa kimataifa dhidi ya Ngaya De Mbe kutoka Uwanja wa Taifa na kupelekwa Amaani visiwani Zanzibar.

Habari za uhakika kutoka ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), zimelieleza DIMBA Jumatano kwamba, Yanga wameandika barua hiyo kuomba mechi hiyo ya marudiano iliyopangwa kupigwa Jumamosi wiki hii ipelekwe Zanzibar, kwa lengo la kuwapa burudani mashabiki wa visiwa hivyo.

Habari hizo zilieleza kuwa awali viongozi waliomba mechi hiyo ichezwa Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, lakini CAF waliwakatalia wakidai kuwa uwanja huo haujakidhi viwango. Pia jana waliandika barua nyingine CAF kuomba kupeleka Uwanja wa Amaan Zanzibar.

Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa, alithibitisha hilo, lakini alisema wameamua kubaki Uwanja wa Taifa baada ya Shirikisho hilo kulikataa ombi lao.

“Tuliomba tubadili uwanja kwa ajili ya kubadili mazingira kwa sababu tumezoeleka sana Uwanja wa taifa, lakini CAF walitujibu hawawezi kubadili kwa kuwa tulikuwa tumeshathibitisha kuutumia Uwanja wa Taifa tangu Januari 2, mwaka huu,” alisema Mkwasa.

Yanga wamejihakikishia nafasi kubwa ya kusonga mbele katika michuano hiyo, baada ya kushinda mabao 5-1 katika mchezo wao wa awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa kwenye Uwanja wa Moroni nchini Comoro.

Katika hatua nyingine, waamuzi wa mchezo huo wanatoka nchini Uganda, huku mwamuzi wa kati akiwa ni Alex Msulumbi, wasaidizi ni Ronald Kakenya na Lee Okello. Wa akiba ni Brian Nsubuga, Kamishina Monnye Nyane kutoka Afrika Kusini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here