SHARE

NA MAREGESI NYAMAKA

YANGA wameimaliza ligi kinyonge baada ya kufungwa mabao 2-0 na Azam FC, mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliochezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Mabao ya Azam katika mchezo huo yalifungwa na Daniel Amoah pamoja na Mudathir Yahya, huku safu ya ushambuliaji ya Yanga iliyoongozwa na Heritier Makambo ikitoka patupu.

Yanga ndio waliokianza kipindi cha kwanza kwa kasi, ambapo dakika ya 16 Kabamba Tshishimbi aliachia shuti kali lililotoka sentimita chache langoni mwa Azam FC.

Dakika ya 31 Obrey Chirwa alifanya kazi ya ziada kuwachambua walinzi wa Yanga, lakini akiwa yeye na kipa alishindwa kuutumbukiza mpira wavuni, huku Yanga nao wakijibu shambulizi hilo dakika ya 39, wakati Makambo akishindwa kuunganisha kwa kichwa krosi ya Yassin Salehe na mpra ukapaa juu na kutoka nje.

Timu hizo zilizidi kushambuliana kwa zamu, Yanga wakitaka kusawazisha, huku Azam nao wakitaka kuongeza bao, ambapo mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika, Wanalambalamba hao walikuwa mbele kwa bao 1-0.

Kipindi cha pili Azam FC walipata bao la mapema dakika ya 49 kupitia kwa Mudathir Yahya, baada ya kuwalamba chenga walinzi wa Yanga na kumchambua kipa Ramadhan Kabwili na kufunga kirahisi.

Licha ya Yanga kutumia kila aina ya mbinu ndani ya uwanja ili kusawazisha, ilishindikana kutokana na Azam kuimarisha ulinzi wao na kulipa kisasi cha mzunguko wa kwanza walipofungwa bao 1-0 na Wanajangwani hao.

Matokeo hayo hayawezi kuathiri chochote kwa Yanga, kwani wanaendelea kubakia nafasi ya pili wakiwa na pointi zao 86, huku Azam nao wakiwa nafasi yao ya tatu, wakifikisha pointi 75.

Kikosi cha Azam FC kilikuwa, Razak Abalora, Lusajo Mwaikenda, Daniel Amoah, Yakubu Mohammed, Agrey Moris, Salmin Hoza, Mudathir Yahya/Frank Domayo, Salum Abubakar, Obrey Chirwa, Donald Ngoma/Dany Lyanga pamoja na Bruce Kangwa.

Yanga: Ramadhan Kabwili, Yassin Haji, Abdalla Haji, Kelvin Yondan, Feisal Salum, Mwinyi Haji
Mrisho Ngassa/Amis Tambwe, Deus Kaseke, Heritier Makambo/Matheo Anthony, Papy Tshishimbi na Gustapha Simon.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here