SHARE

Na Winfrida Mtoi

UONGOZI wa klabu ya Yanga umeanika mpango kazi uliobeba mambo matano ambayo wamepanga kuyatekeleza mara tu Serikali itakaporuhusu kurejea tena kwa kivumbi cha Ligi Kuu Tanzania Bara na mikusanyiko ya masuala ya michezo.

Itakumbukwa ni takribani miezi miwili sasa tangu Serikali imepiga marufuku mikusanyiko ya aina yoyote nchini ukiwa ni mkakati wa kupambana na mlipuko wa maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa corona.

Kuibuka kwa ugonjwa huo kunatajwa kuzima mipango ya maendeleo ya klabu hiyo iliyokuwa imepangwa kutekelezwa chini ya Mwenyekiti Dkt. Mshindo Msolla ambapo sasa uongozi wa klabu hiyo umekaa mguu sawa.

Habari njema ni kwamba, sasa Ligi Kuu Tanzania Bara iko mbioni kurudi ambapo uongozi wa Yanga umeanika vipaumbele vitano ambavyo fasta wanakwenda kuvitekeleza ili kutimiza ahadi yao kwa wanachama kuifanya klabu hiyo kuwa ya kisasa.

*Mchakato wa mabadiliko

Katika kipindi ambacho ligi itakuwa inaendelea,Yanga imepanga itakuwa inatambulisha na kutoa taarifa za hatua iliyofikia kuhusu mchakato wa mabadiliko.

Mchakato wa mabadiliko wa uendeshaji wa klabu hiyo, ulikuwa haujafikia hatua ya wanachama kupewa nafasi ya kuchangia maoni yao, lakini baada ya kukamilika andiko la awali mambo yatarajia kwenda kwa kasi.

Pia wataalamu kutoka La Liga nchini Hispania, walishindwa kufika kuanza kazi kutokana na mlipuko wa virusi vya corona, lakini sasa tayari makubaliano ya kusaini mkataba yamefikiwa.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Sheria na Wanachama wa Yanga, Simon Patrick, kila kitu kimekamilika na muda wowote mkataba huo wa awali wa kuelekea mabadiliko utasainiwa.

Alisema, watu wa La Liga watakuwa wanasimamia na kusaidia mchakato ili kwenda katika mfumo unaotakiwa.

“Mkataba umekamilika, umepitiwa na pande zote mbili na tumekubaliana mambo yote ya msingi, kinachosubiriwa ni kusaini, tunasubiri wenzetu kutoka Hispania wathibitishe tarehe rasmi tutakayofanya tukio hili, tunaamini itakuwa wiki za karibuni,” alisema Simon.

*Nyota wapya kuanza kuwasili

Endapo hali ya maambukizi ya corona itaendelea kupungua, nyota wapya wa kimataifa waliopo katika mpango wa usajili wa Yanga wanatarajia kuanza kuwasili nchini ili kukamilisha usajili wao.

Nyota hao wa kimataifa wanakuja nchini kukamilisha taratibu za usajili ikiwamo kusaini mikataba kwa sababu kocha mkuu wa timu hiyo, Luc Eymael, naye atakuwa tayari ameshawasili nchini.

Ofisa Mhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz, amesema ligi itakapoanza watakuwa wamekamilisha kwa asilimia 70 mipango yao mingi ikiwamo usajili wa kimataifa na wa ndani ili kujiwinda na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa.

Tayari mdhamini wa klabu hiyo, kampuni ya GSM, imeshatangaza wamepanga kusajili mchezaji yoyote bila kujali gharama aliyonayo kwani wamedhamiria kuiona Yanga ikifanya makubwa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa.

*Ujenzi wa uwanja

Ligi itakapokuwa inaendelea, ujenzi wa uwanja kwenye eneo lao la Kigamboni utakuwa umefikia hatua nzuri zaidi kwa sababu Kamati ya Ujenzi na Miundombinu imeshakamilisha ripoti ya muundo wa uwanja huo.

Wanayanga wengi wanatamani kuona ujenzi huo umeanza rasmi kutokana na kejeli wanazopata kutoka kwa watani zao Simba ambao wanamiliki uwanja wa mazoezi kule Bunju nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Kampuni ya GSM tayari wametia mkono mpango kazi wa ujenzi wa uwanja huo ambapo wameahidi kuangusha bonge la uwanja wa kisasa utakaokuwa kitega uchumi kwa klabu hiyo.

*Kufuta makundi

Wakati klabuni hapo ikidaiwa kuwepo kwa makundi ndani ya uongozi, Wanajangwani hao wameweka mambo sawa na wanatarajia kurudi wakiwa katika umoja na nguvu mpya.

Dkt. Msolla alisema uongozi upo imara, hakuna tatizo lolote na kwamba wanapiga kazi kwa ushirikiano mkubwa na wadhamini wao, lengo likiwa ni kufikisha Yanga kule inakohitajika, kila mmoja atashiriki katika mabadiliko na marekebisho ya katiba ya mwaka 2010.

*Mikakati kabambe Kombe la FA

Baada kupoteza matumaini ya kuchukua ubingwa Ligi Kuu Tanzania Bara, Wanajangwani hao wanarudi na nguvu mpya katika michuano ya Kombe la Shirikisho Tanzania.

Yanga imejipanga vilivyo kuonesha ubabe kutokana na kupata muda mrefu wakupitia makosa na kuyafanyia kazi kwa pamoja, uongozi na benchi la ufundi ili kuhakikisha wanatwaa taji hilo na kuweka kibindoni tiketi ya kucheza michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here