SHARE

NA TIMA SIKILO

UZALENDO umemshinda kocha wa zamani wa Yanga, Mwinyi Zahera, na kuamua kutamka hadharani kwamba Wanajangwani hao wamelamba dume baada ya kufanikiwa kuinasa saini ya kiungo mshambuliaji, Owen Bonyanga Ituku, kutoka TP Mazembe ya DR Congo.

Zahera ambaye alitupiwa virago Yanga kwa madai ya kuishiwa mbinu, alisema mchezaji huyo waliyemsajili ni mzuri sana hivyo kama wataweza kumtumia ipasavyo hawatajutia maamuzi yao.

Alisema kiungo huyo mshambuliaji hana mambo mengi sana uwanjani zaidi ya kupokea mipira na kutoa pasi za uhakika, akipenda zaidi kusukuma mashambulizi mbele na kama washambuliaji wa Yanga watakuwa makini watapachika mabao ya kutosha.

“Namjua, ni mchezaji mzuri sana. Kama Yanga wataweza kumtumia watafaidi kwani hana mambo mengi sana anapokuwa uwanjani zaidi ya kuhitaji kupeleka mbele mashambulizi.

“Binafsi naamini safu ya ushambuliaji ya Yanga ikiwa makini inaweza ikapachika mabao mengi kwani huyu mchezaji waliyemsajili sio mchoyo hata kutoa pasi za mwisho, nawatabiria makubwa,” alisema.

Kuhusu Mbelgiji, Luc Eymael, ambaye ndiye sasa kocha mkuu wa kikosi hicho akichukua mikoba yake, Zahera alisema naye ni kocha mzuri kwa sababu amefundisha timu nyingi kubwa zikiwamo za Congo.

“Ni kocha mzuri kama watamtunza kwani amefundisha timu mbalimbali kubwa ikiwamo AS Vita. Kocha yeyote akipewa mahitaji yake anaweza kufanya vizuri na kama hatapewa anaweza akaonekana mbaya ndiyo maana nasema wakimpa mahitaji yote atakayoyahitaji watafanikiwa,” alisema.

Baadhi ya timu ambazo kocha huyo amewahi kuzinoa ni AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Missile ya Gabon, JS Kairouan ya Tunisia, Al Nasr ya Dubai, Al Merreikh ya Sudan, Polokwane City, Black Leopard pamoja na Free State Stars zote za Afrika Kusini, Tala’ea El Gaish ya Misri, AFC Leopards ya Kenya na Rayon Sport ya Rwanda.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here